Breaking News

TAWA YASHEREKEA SIKU YA WANYAMAPORI DUNIANI KWA KUTOA MISAADA NA ELIMU YA UHIFADHI

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Kanda ya Magharibi leo Machi 3, 2025 imesherehekea Siku ya Wanyamapori Duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na uhifadhi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kulinda wanyamapori na mazingira.

Katika maadhimisho hayo, Kanda hiyo ilitoa misaada ya vyakula kwa wanafunzi wenye uhitaji kutoka Shule ya Wanafunzi wenye changamoto ya uoni ya Furaha ikiwemo mchele, unga, mafuta, sukari na sabuni vyote vikiwa na thamani ya shillingi millioni moja. 

Misaada hii imelenga kuwasaidia wanafunzi hao na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Vilevile TAWA ilitembelea Shule ya Sekondari Fundikila na kutoa miche 4000 ya miti ya matunda ya muda mfupi, ikihamasisha upandaji wa miti na kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira. Shule ya Sekondari Kanyenye nayo ilipokea miche 2000 mingine, kama sehemu ya juhudi za kukuza mazingira bora na endelevu kwa jamii.

Akikabidhi misaada hiyo na miche ya miti Kaimu Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Magharibi Lupondije Nyanda ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora kushirikiana na Serikali katika jitihada za kulinda rasilimali wanyamapori ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira yao huku akiwahamasisha kutembelea vivutio vya utalii hususani bustani ya wanyamapori hai almaarufu Tabora ZOO.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani Kitaifa yaliyanyika katika viwanja vya ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Dodoma mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana





No comments