Breaking News

JESHI LA POLISI LAFANIKIWA KUMUOKOA MTOTO ALIYETEKWA

Dar es salaam - Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kumrejesha mikononi mwa wazazi wake mtoto wa kiume wa miaka 8 anayesoma shule ya Msingi Mbezi Ubungo Dar es Salaam aliyetekwa Machi 6 , 2025 na Stanley Dismas Ulaya (18) Mkazi wa Kata ya Nguruka Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi SACP Muliro Jumanne Muliro amesema Machi 8, 2025 Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa na baadae kumjeruhi kwa risasi alipojaribu kutoroka chini ya ulinzi.

Alisema siku ya tukio Askari walijaribu kumstua kwa risasi za juu lakini alikaidi ikabidi kitendo kilichopelekea apigwe risasi ya paja na kujeruhiwa hivyo yuko Hospitali Chini ya Jeshi la Polisi akipatiwa matibabu.

“Mtuhumiwa alitekeleza tukio hilo Machi 6, 2025 wakati mtoto huyo aliposhuka katika daladala akienda shule kabla ya kuingia katika geti la Shule alikamatwa na mtuhumiwa na kumpeleka hadi Bagamoyo Pwani ambako mtuhumiwa alikaa nae vichakani huku akitumia namba ya simu ya mzazi iliyokuwa kwenye madaftari kuipiga huku akidai pesa ili amuachie na asimdhuru mtoto huyo na wasipotuma watafuta maiti,”. Alisema Kamanda Muliro

SACP Muliro amebainisha kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaammara baada ya kupata taarifa juu ya tukio hilo lilifanya kazi kubwa ya ziada ya ufuatiliaji ambapo Machi 8, 2025 majira ya saa 01:00 usiku mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi Oysterbay na alijaribu kutoroka kwa kukimbia alipigwa risasi mguuni na kwenye paja hivyo kufanikiwa kumzibiti mtuhumiwa amepelekwa hospitali Kwa matibabu akiwa na hali mbaya.

Kwa upande wa Mzazi wa Mtoto huyo bwana Johnson Koranya amesema siku ya tukio kama kawaida alimpeleka mtoto shuleni na kumuacha kituo cha mabus karibu na shule lakini ilipofika jioni mtoto hakurejea nyumbani ndipo walipoanza kumtafuta.

Bw. Koranya kufatia hali hiyo walichukua hatua ya kumtafuta mwalimu na kumuulizia mtoto, mwalimu ndipo alimpatia namba ya mtu aliyekuwa akimsumbua akimtaka mzazi wa mtoto huyo.

Hivyo Koranya amesema baada ya kuwasiliana Kwa namba hiyo aliambiwa atume kiasi cha shilingi Milioni 50 ndiyo mtoto aachiliwe asipotuma atakuta maiti ambapo aliamua kwenda kuripoti kituo cha Polisi ili asaidiwe.

"Kwa dhati kabisa napenda kutoa shukran kwa jeshi la polisi janda maalum ya Dar es salaam kwa jitihada za haraka ambazo zimepelekea kupatikana kwa mwanangu akiwa hai na Afya njema". Alisema Bw. Koranya. 

No comments