Breaking News

WANAJESHI WAWILI WA JWTZ WAFARIKI DUNIA DRC

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema kuwa limewapoteza Askari wake wawili (02) na wengine wanne (04) wamejeruhiwa Kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya SAKE na GOMA Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo (DRC) yaliyofanywa na Waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari 2025.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Kanali Gaudentius Gervas Ilonda imeeleza kuwa Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma na Taratibu za kuisafirisha miili ya Marehemu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretarieti ya SADC.

Askari hao walikuwa ni miongoni mwa askari wanaolinda amani chini ya Mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika eneo la Mashariki mwa DRC (SAMDRC), eneo ambalo limekumbwa na mgogoro uliozua mashambulio kati ya waasi wa M23 wanaopambana na Jeshi la DRC (FARDC) katika maeneo hayo.

"Aidha, vikundi vyetu vilivyopo nchini DRC vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya Uongozi wa SADC." - Amesema Kanali Gaudentius Gervas Ilonda.


 

No comments