MATWEBE: SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMETUHESHIMISHA JUMIKITA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Kimtandao Tanzania (JUMIKITA), Shaabani Matwebe, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewapatia waandishi wa habari wa mtandaoni nafasi kubwa ya kushiriki katika shughuli za kitaifa, tofauti na ilivyokuwa awali.
Akizungumza katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Star TV, Matwebe alisema juhudi za JUMIKITA zimechangia kuboresha hadhi ya waandishi wa habari wa mtandaoni na kuwawezesha kushiriki kwenye matukio muhimu ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na misafara ya viongozi wakuu wa serikali.
“Katika kitu ambacho niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita ni kwamba sisi baada ya kuunda jumuiya na kutafuta njia mbalimbali za kushirikiana na serikali, tumepokelewa vizuri. Waandishi wa habari wa mtandaoni sasa wanashiriki katika misafara mikubwa ya viongozi, jambo ambalo zamani halikuwepo,” alisema Matwebe.
JUMIKITA YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA MTANDAONI
Matwebe alieleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa JUMIKITA mwaka 2021, waandishi wa habari wa mtandaoni walikumbwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kutotambuliwa rasmi na taasisi mbalimbali za serikali.
“Tuna changamoto nyingi, lakini kupitia JUMIKITA, tumefanikiwa kuwaunganisha waandishi wa mtandaoni na taasisi za serikali, jambo ambalo limewapa heshima na kutambuliwa katika sekta ya habari,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa kupitia juhudi za jumuiya hiyo, waandishi wengi wa habari wa mtandaoni wamepata mafunzo ya maadili ya uandishi wa habari, huku wengine wakipata fursa ya kushirikiana na taasisi za serikali na sekta binafsi.
Aidha, Matwebe aliwataka waandishi wa habari wa mtandaoni kutumia vyema fursa zinazotolewa na serikali kwa kuhakikisha wanazingatia weledi na maadili katika kazi zao.
“Sera za serikali ni nzuri, na toka Awamu ya Sita imeingia madarakani, tumeweza kufanya kazi kwa uhuru zaidi. Hata hivyo, waandishi wa habari wa mitandaoni wanapaswa kuwa makini, kufuata maadili na kuhakikisha wanatoa habari sahihi na zenye ukweli,” alisisitiza.
JUMIKITA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha waandishi wa habari wa mtandaoni wanapata mazingira bora ya kazi, fursa za mafunzo na ulinzi wa haki zao.
No comments