Breaking News

RAIS DKT. SAMIA ALIHUTUBIA TAIFA, AELEZA MIKAKATI NA MAFANIKIO YA MWAKA 2024

Zanzibar, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo amelihutubia taifa na kutoa muhtasari wa mafanikio na mikakati ya serikali kwa mwaka 2024. Akianza hotuba yake, Rais alieleza kuwa mwaka huu umekuwa wa neema na mafanikio makubwa kwa taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kumshukuru Mungu kwa hatua zote zilizopigwa katika kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza wakati akilihutubia taifa katika Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar Rais alitaja mafanikio ya kisiasa, akieleza kuwa mwaka huu Tanzania ilifanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na utulivu. Kwa mara ya kwanza, wagombea ambao hawakuwa na washindani walilazimika kupata ridhaa ya wananchi kupitia kura ya “Ndiyo” au “Hapana.” Alibainisha kuwa hatua hii imeondoa utaratibu wa kupita bila kupingwa, jambo ambalo limeimarisha demokrasia nchini.

Katika hotuba yake, Rais alieleza kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 4.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023. Aidha, mfumuko wa bei uliendelea kudhibitiwa ndani ya lengo la asilimia 3, huku deni la taifa likibakia himilivu.

Kuhusu uwekezaji, Rais alieleza kuwa Tanzania imesajili miradi 865 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 7.7 kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Miradi hii inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 205,000. Aidha, Mamlaka ya EPZA imetoa vibali kwa viwanda 15 vipya vyenye thamani ya Dola milioni 235, ambavyo vitazalisha ajira karibu 6,000 na bidhaa za mauzo nje zenye thamani ya Dola milioni 94 kila mwaka.

Kwa upande wa mapato, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya Shilingi trilioni 21.276 kati ya Januari na Oktoba 2024, sawa na asilimia 99.3 ya lengo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Rais alibainisha kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika kujenga uchumi wa kidijitali kwa kuunda Wizara maalum ya TEHAMA na kuzindua Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali. Mkakati huu unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anatambulika kupitia Jamii Namba, itakayotolewa na NIDA.

Rais alizungumzia mafanikio ya kidiplomasia, akibainisha ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa G20 na mafanikio yake. Aidha, alitoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, ambaye alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika.

Akizungumzia Ziara za kimataifa pia amesema zilileta mafanikio, ikiwemo Jamhuri ya Korea ambapo zilipatikana Dola bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa vituo vya reli, anga, umeme, madini, na kongani ya viwanda Bagamoyo.

China: Ufunguzi wa masoko kwa bidhaa za kilimo na mazao ya baharini, na makubaliano ya kufufua reli ya TAZARA.

Rais alikumbusha kuwa Tanzania ilipokea Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, ambapo taifa liliendesha kwa mafanikio uangalizi wa chaguzi katika nchi za Botswana, Mauritius, Msumbiji, na Namibia.

Kwa kumalizia, Rais alisisitiza kuwa mafanikio ya mwaka 2024 yanatoa msingi imara kwa maendeleo ya taifa katika nyanja za uchumi, demokrasia, kidijitali, na diplomasia ya kimataifa. 

No comments