Breaking News

MHE. CHANA AWAFUNDA MAAFISA WANYAMAPORI

Na Saidi Lufune - Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Hazara Chana amewataka Maafisa Wanyamapori wote nchini kuchukua hatua madhubuti ya kulinda na kuhifadhi wanyapori ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kupambana na changamoto za ujangili.

Mhe. Chana ameyasema haya leo Desemba 03, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi semina ya siku mbili inayowahusisha Maafisa Wanyamapori kutoka wilaya 138 hapa nchini.

Amewataka Maafisa Wanyamapori hao kutoa ushauri kwenye vikao vya Kamati za madiwani zinazoshughulikia Uchumi na Mazingira kwenye Halimashauri wanazotoka ili kuimarisha uhifadhi.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zinazoongoza duniani kwa kuwa na bioanuai nyingi kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia

Amesema kupitia sekta hiyo kila mwaka imechangia kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana takriban milioni 1.6 na hivyo kuwataka maafisa wanyapori nchini kufuata maadili ya kazi zao katika kulinda na kuthamini rasilimali hiyo ikiwemo kutojihusisha na vitendo vya ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo

“Nipende kuwakumbusha kuwa waadilifu na tuzingatie maadili ya utumishi wa umma ikiwa ni pamoja kutojihusisha na vitendo vya ujangili, rushwa na wizi kwa faida yenu wenyewe na kwaq faida ya umma uliowaamini kusimamia rasilimali” Amesisitiza Mhe. Chana
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula amewaomba Maafisa Wanyamapori wote kuzingatia mafunzo yanayotolewa na Wizara.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili ana Utalii Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba, amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa wananyamapori ikiwa ni pamoja na kuandaa sera, kanuni, mikakati na miongozo mbalimbali ya kulinda rasilimali za Wanyama Pori 

“Wizara inatambua mchango mkubwa wa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya katika kutekeleza sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 na Sheria ya Wanyamapori Sura ya 283.” Amesema Kamishna Wakulyamba
Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kisheria unaowezesha uanzishwaji wa maeneo Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori ili kutambua shughuli za uhifadhi kwenye maeneo hayo sambamba na kutatua chngamoto zinazowakabili za wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt Alexander Lebora amefafanua kuwa katika semina hii washiriki watafundishwa mfumo wa kielektroniki wa kukusanya taarifa.

No comments