Breaking News

MBOWE RASMI ATANGAZA NIA KUTETEA UENYEKITI CHADEMA

Dar es salaam - Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametangaza nia yake ya kugombea  nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika ngazi ya Taifa.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari  Jjini Dar es Salaam, Mbowe amesema ametafakari kwa kina kuhusu kuachia nafasi ya uenyekiti huku akimkaribisha yeyote anayetaka kugombea kiti hicho.

"Nimetafakari kwa kina sana. Nimesema mara nyingi nilitamani kuondoka, lakini siwezi kuondoka katikati ya minyukano iliyopo. CHADEMA nipo, nitakuwepo, nitagombea nafasi ya uenyekiti ngazi ya Taifa. Anayetaka kugombea, tukutane kwenye boksi.", amesema Mbowe.
Mbowe amekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA kwa miaka mingi, amekuwa kipenzi cha wengi kutokana na msimamo wake wa kupigania demokrasia na haki za wananchi, licha ya changamoto kadhaa za kisiasa zinazokikumba chama hicho.

Kwa upande mwingine, Tundu Lissu, ambaye ni mwanasiasa maarufu na miongoni mwa viongozi waandamizi wa CHADEMA, pia ametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya uenyekiti.

 Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA ambaye aliishi uhamishoni baada ya tukio la kupigwa risasi mwaka 2017, amekuwa na sauti kubwa katika upinzani na alikubali kurudi nchini kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa chama hicho.
Tangazo la Lissu la kugombea uenyekiti limeleta ushindani mkubwa, huku kukiwa na mchuano mkali wa kisiasa ndani ya CHADEMA.

Uchaguzi wa uenyekiti CHADEMA unatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa mustakabali wa chama hicho, kwani Mbowe na Lissu ni miongoni mwa viongozi wanaoongoza kwa kuungwa mkono na wanachama wengi, na kila mmoja ana mtindo na maono tofauti kuhusu mwelekeo wa chama hicho.

No comments