WAZIRI MAJALIWA KUFUNGUA KONGAMANO LA NANE LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) wameandaa kongamano la nane (8) litakalowaleta pamoja Wadau takribani 700 wa masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya uwezeshwaji wa wananchi pamoja na changamoto zake jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa amesema wadau hao watakutana kwa siku mbili Disemba Desemba 3 na 4 2024 kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya uwezeshwaji wa wananchi pamoja na changamoto wanazokutana nazo.
Amesema kongamano hilo litahusisha wizara, mashirika, wakala na taasisi za Serikali, taasisi binafsi chini ya mwamvuli wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), mikoa, halmashauri, wajasiriamali, taasisi za fedha, taasisi za elimu, watafiti, wawekezaji pamoja na wadau wengine wa masuala ya uwezeshaji.
Ameeleza kuwa kupitia midahalo mbalimbali itakayofanyika katika kongamano hilo, watajadili namna ambavyo wananchi wanaweza kunufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza kujikwamua kiuchumi.
Pia ameeleza kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo linaloongozwa na kauli mbiu isemayo: Uwezeshaji wananchi kiuchumi ni msingi wa maendeleo ya Tanzania
"Kongamano litatoa pia fursa ya kutathmini utekelezaji wa sera ya uwezeshaji pamoja na taarifa mbalimbali ya utekelezaji wa mambo yaliyokuwa kwenye kongamano la saba, "amesema.
Ameongeza kuwa wakati wa kongamano, tuzo pia zitatolewa kwa wote waliofanya vizuri ikiwemo mkoa uliofanya vizuri, wajasiriamali na taasisi mbalimbali za uwezeshaji, kwani mafanikio mengi yameshapatikana chini ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi
No comments