Breaking News

TUZO YA USIKU WA MADINI 2023 YAMPA HAMASA KUANZISHA KAMPUNI

Tuzo ya Mwanamke Bora katika Sekta ya Madini Mwaka 2023 ilikwenda kwa Mwanadada Leminatha Cornel Kabigumila mama wa Watoto wawili mwenye umri wa miaka 38. Kabla ya kushinda tuzo hiyo, Leminatha alikuwa akimiliki jumla ya leseni 4 za uchimbaji mdogo wa madini ya Bati (Tin) 

Tuzo hiyo ilimpa hamasa kubwa ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini na sasa ameanzisha kampuni inayojulikana kama Rare Mining East Africa LTD yenye jumla ya leseni 21 za uchimbaji mdogo wa Madini ya bati na leseni 74 zipo kwa jina lake. 

Ili kupata leseni hizo, ilimlazimu Bi. Leminatha kulipa kiasi cha shilingi milioni 150 Serikalini ikiwa ni ada za leseni baada ya wamiliki wa awali kushindwa kuzilipia na kuziendeleza. Pia, alilipia leseni 33 za mdaiwa mwingine kwa kiasi cha shilingi milioni 120 na kuziendeleza. Kwa kifupi ni kwamba hivi sasa mwanamama huyu anamiliki jumla ya leseni 95 za uchimbaji mdogo wa madini ya bati (Tin) na 1 ya dhahabu zote zikiwa hai na zinaendelezwa.

‘’ Ile tuzo ilinipa hamasa kubwa na nguvu za kusonga mbele zaidi, nilijishukuru mwenyewe kwanza, kwa kutokukata tamaa. Sikuwa na kampuni lakini sasa hivi nina kampuni yangu na ina leseni 21 za uchimbaji wa madini ya bati. Nimehamasisha watu kulipa madeni ya Serikali zaidi ya shilingi milioni 300 waliokuwa wadaiwa sugu. Furaha yangu ni kwamba nilianzia chini sana kuelekea juu, maana nilianza kwa kuuza maziwa na mandazi, baada ya kufiwa na mzazi mwenzangu, sikupewa chochote, lakini nilisonga mbele kwa sababu nilikuwa na picha kubwa. Ile tuzo imefanya nianzishe NGO’s na kuanza kuishi maisha ya mguso katika jamii yangu,’’ anasema Leminatha. 

Leminatha alitunukiwa tuzo hiyo katika hafla ya Usiku wa Madini inayofanyika kila mwaka wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania. Usiku wa Madini umekuwa ukitumika kama sehemu ya kutambua mchango wa wadau mbalimbali waliofanya vizuri katika Sekta ya Madini kupitia vipengele mbalimbali kama uchangiaji bora wa mapato kwa Serikali, uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, ushirikishaji watanzania, uongezaji thamani madini ambayo kwa pamoja yamechangia katika ukuaji na maendeleo ya sekta ya madini nchini.

 Pia, Usiku huo huenda sambamba na onesho maalum la madini ya vito na usonara linalolenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye madini ya vito pamoja na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za mapambo zinazotengenezwa nchini.

Akielezea historia yake ya uchimbaji, Leminatha anasema alianza shughuli zake mwaka 2017 katika kijiji cha Mwime, Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo alikuwa akichimba na kukusanya madini ya dhahabu. Mnamo mwaka 2021 alielekeza shughuli zake Mkoani Kagera Wilaya ya Kyerwa ambapo anachimba madini ya bati (Tin) katika leseni zake na kuuza kwa wafanyabiashara wakubwa (dealers) kupitia Soko la Madini Kyerwa. Anaongeza kwamba amejielekeza kwenye madini ya bati kutokana na mahitaji ya madini hayo duniani hivi sasa yanauzika bila kikwazo. 

‘’ Kilichonisukuma kuwekeza sekta ya madini ni kwa sababu mimi mwenyewe ninapenda madini hivyo niliamini ninaweza kufanikiwa katika sekta ya madini. Ninafanikiwa kwa sababu ya Sera na Sheria rafiki katika sekta ya madini. Pia ninapata ushauri sahihi kutoka kwa viongozi wa Serikali ambao wanaonishauri vyema na kupata mafanikio. Kwa ujumla ninafurahia uwekezaji wangu kwenye Sekta ya Madini kutokana na namna serikali inavyotuongoza vema,’’ anasema Leminatha. 

‘’Kwanza ninapenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, ninaishukuru Serikali kwa kutambua nafasi ya kila mchimbaji hususan sisi wanawake. Ninamshukuru Rais wangu Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwangu mimi siyo Rais tu bali ni mwalimu na darasa linaloishi, ninawashukuru Maafisa Madini wote na hususan Samwel Shoo kwa kuniamini na kunisaidia kupata leseni za madini na sasa nina jumla ya leseni 95 zote zikiwa zinafanya kazi,’’ anaongeza Leminatha.

Leminatha anapenda kuwaasa wanawake wengine kutambua kwamba kazi ni muhimu na inaongeza thamani ya mwanamke na ana amini kuwa mwanamke ni mzalishaji mzuri kutokana na nguvu aliyonayo pindi anaporuhusu ifanye kazi, ‘’ mwanamke nakushauri fanya lolote kwa moyo wa kupenda na tafuta maarifa kwenye hilo eneo, nakuhakikishia matafanikio yatakutafuta, hutoyatafuta na ukifanya kazi utaleta suluhu na mafanikio makubwa kwenye familia yako. Tambua watoto wanajifunza kwetu sana kuliko kwa baba zao, je wanajifunza nini kwako kama mama,’’? anaeleza. 

Akizungumzia changamoto za uwekezaji wake anasema zipo na hazikosekani na kuzitaja kuwa ni pamoja na kupanda na kushuka kwa bei za madini hayo, hata hivyo Leminatha anasema changamoto hiyo inampa ari ya kusonga mbele kwasababu anapenda kufanya kazi na kujituma ili kuacha alama katika vizazi vijavyo, ‘’sipendi kubweteka, uwajibikaji unanipa nguvu ya kujivunia kuzaliwa Tanzania, na kubwa kabisa ni furaha yangu pale ninapochangia pato la nchi yangu,’’ anasema Leminatha. 

Akizungumzia mipango yake siku za usoni anasema ni kusafirisha madini kwenda soko la dunia na baadaye kujenga viwanda vyake hapa nchini na kutumia madini kutengeneza bidhaa mbalimbali za madini yanayozalishwa nchini zenye nembo yake ya LEM-NES INTERNATIONAL LTD, na kuongeza naamini hili litatamia,’’.

Mwaka 2020 Tanzania ilijiunga na mpango wa Nchi za Maziwa Makuu wa kuhakikisha madini ya 3Ts yaani (tin – bati, tantalum na walfranite) yanazalishwa kwenye vyanzo visivyo na migogoro ya kivita na vinavyokidhi viwango vya chini vya kijamii (mfano: hakuna watoto wanaofanya kazi) maarufu kama ICGLR. Kutokana na Tanzania kujiunga kwenye mfumo huo (ICGLR) wachimbaji wa Tin wamepata fursa ya kuuza madini ya Tin nchi yoyote duniani na kupata uhakika wa masoko kutokana na cheti hicho cha ICGLR kuyatambulisha rasmi. 

Soko la madini ya Tin lilizinduliwa mwezi Mei, 2019 mkoani Kagera Wilaya ya Kyerwa. Madini ya bati yana matumizi mbalimbali ikiwemo kutumika kuunganisha vitu mbalimbali kama mabomba ya chuma na metali (Steel/ Metal), mifumo ya umeme (electric circuit), mifumo ya kielektroniki ya simu, vyuma vya reli, mifumo ya ndege na mifumo ya lifti za umeme kwenye ghorofa. 

Pia, madini ya hayo hutumika kuzuia kutu kwenye vyombo vya kuhifadhia chakula (Tin plated steel containers au Tin cans food storage containers) kwa muungano wa madini ya chuma. Tin vilevile hutumika kuzuia kutu kwenye mabati ya kujengea nyumba (Iron sheet tin coating). 

Leminatha amekuwa mwanamke wa mfano kati ya wengi waliowekeza katika mnyororo wa shughuli mbalimbali za madini. Ili kuhakikisha wanawake wengi zaidi na vijana wanashiriki katika uchumi wa madini, katika Mwaka wa Fedha 2024/25, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeandaa program maalum ya Mining For Brighter Tomorrow (MBT) inayolenga kuwaendeleza vijana na wanawake wachimbaji kwa kuwapatia leseni za maeneo ya kuchimba, vifaa, magari na mitambo.
 

No comments