Breaking News

TANZANIA YAIELEZA UN WANANCHI WAKE WOTE NI SAWA MBELE YA SHERIA

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Profesa Hamis Malebo akizungumza katika Mkutano unaoendelea wa Umoja wa Mataifa Jijini New York Marekani.

Mwandishi Maalum, New York, Marekani
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilihudhuria kikao cha Kamati ya 3 ya Haki za Watu wa Asili wakati wa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea New York, Marekani.
Prof. Hamisi M. Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya taifa ya UNESCO ya Tanzania alijibu kwa niaba ya Serikali taarifa ya mada kuhusu "Watu wa Asili wanaohamishwa" iliyowasilishwa na Mwandishi Maalum wa Haki za Watu wa Asili, Bw. José Francisco Calí Tzay.

Prof. Malebo aliuambia mkutano huo kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezingatia Taarifa ya Mwandishi Maalum na inasisitiza msimamo wake kuwa Tanzania haikubaliani na dhana ya watu wa asili inayopigiwa chapuo na mfumo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa. Alisisitiza kuwa, si sahihi kujadili haki ya kumiliki na kusimamia ardhi pamoja na uhamishaji wa hiari unaoendelea wa wakazi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro chini ya mwamvuli wa ‘haki za watu wa asili’ kwa kuwa Tanzania haina watu wa asili.

Kuhusu umilikaji wa ardhi, Prof. Malebo aliueleza mkutano huo kuwa, ili kuweka mambo katika muktadha sahihi, ni busara kuufahamu mfumo wa umiliki wa ardhi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ardhi inamilikiwa na umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini. Mtu anapewa haki ya kumiliki kwa muda maalum kwani sio mfumo wa kushikilia ardhi bure bila malipo. Hakuna ardhi ya kibinafsi wala ardhi ya kabila wala ardhi ya mababu nchini Tanzania. Kwa hiyo, siyo sahihi kudai kwamba, kuna Watu wa Asili ndani ya nchi ya Tanzania na kwamba wana haki za kipekee na maalum za kumiliki ardhi. Kwa hakika, hakuna kabila lolote kati ya zaidi ya 120 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloweza kudai umiliki wa kikabila juu ya ardhi, hakuna utaratibu kama huo nchini Tanzania.

Kuhusu madai ya kuondolewa kwa Wamaasai kwa nguvu, Prof. Malebo alikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapinga na kukanusha tuhuma zote za kuondoa wananchi kwa nguvu katika Hifadhi ya Ngorongoro (NCA). Akasisitiza kuwa kinachofanyika huko ni Mpango wa Kuhama kwa Hiari kufuatia mapendekezo kutoka kwa mapitio shirikishi ya Mfumo wa Matumizi Mseto wa Ardhi (MLUM). Prof. Malebo alisisitiza kuwa, Serikali ilizingatia kanuni ya Kupata Ridhaa Huru, Kabla na Kwa Kutaarifiwa (FPIC) katika utekelezaji wa Mpango wa Kuhama kwa Hiari. Watu wanaoishi katika NCA wana uhuru wa kutuma maombi rasmi ya kuhama na kujiorodhesha kuhamishwa kwenda nje ya eneo hilo. Serikali inasisitiza kuwa kuna mpango wa kuhama kwa hiari ambapo tangu ulipoanza Juni 2022 hadi Juni 2024 jumla ya kaya 1,519 zenye watu 9,251 na mifugo 38,7894 zimehama kwa hiari kutoka Ngorongoro na kwenda maeneo mengine. Hakuna shuruti ya aina yoyote inayotumika kuwahamisha wakaazi wa Ngorongoro.

Kuhama kwa hiari hufanyika tu baada ya mwananchi kuomba baada ya kuelimishwa naye akaridhia kuhama akiwa ameeleweshwa kuhusu mchakato, fidia na bakshishi kutokana na uamuzi huo. Zaidi ya hayo, wakaaji wako huru kuhamia maeneo yaliyotengwa na pia maeneo mengine wanayochagua wenyewe ndani ya nchi. Maeneo yaliyotengwa yanafanana na Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuzingatia mazingira na upatikanaji wa mimea mahsusi inayotumika na Wamaasai katika maeneo ya kitamaduni kwa matambiko na sherehe za jadi. Wakazi wanaoishi katika maeneo yaliyochaguliwa pia walikuwa wakazi wa Ngorongoro na walihama wenyewe kwa hiari miaka mingi iliyopita kutoka Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti na kufanikiwa kumudu mazingira na kuendelea kufuga kitamaduni na kuendesha mila na tamaduni zao bila kikwazo. Aidha, watu hao ni watu wale wale wa jamii ambayo inahama sasa kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda eneo hilo na wanahusiana kiufugaji, lugha na utamaduni.
Prof. Malebo aliuambia mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuwa, mpango wa kuhama kwa hiari ulipangwa kwa kuzingatia haki za msingi za binadamu zilizo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na Matamko mengineyo yaliyoridhiwa na Tanzania. Katika mpango huo, serikali imejenga nyumba za kisasa kwa familia hizo na kila nyumba iko kwenye eneo la ekari mbili na nusu ili kuwaruhusu kufuga mifugo kama katika eneo wanakotoka. Serikali imetenga ekari tano za ardhi kwa kila familia kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

 Wakati huo huo kuna eneo kubwa limetengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo, huduma za mifugo, umeme, mitandao ya mawasiliano, maji, shule, vituo vya afya na kituo cha polisi kwa madhumuni ya usalama. Wakati wa kuhama kwa hiari, serikali inagharamia usafiri, upakiaji na upakuaji pamoja na kuwapatia chakula kwa kipindi cha miezi 18.

Prof. Malebo aliukumbusha mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku zote imekuwa wazi na jumuiya ya kimataifa kuhusu changamoto zinazowakabili wananchi wake katika Hifadhi ya Ngorongoro. NCA ilianzishwa mwaka wa 1959 ikiwa na wastani wa watu 8,000 ambao walikaa katika kilometa za mraba 6.4 za ardhi. Hata hivyo, kufikia mwaka 2021 idadi ya wakazi ilifikia watu 110,000 wanaokalia kilometa za mraba 3,700 za ardhi, mifugo iliongezeka kutoka 260,000 mwaka 1959 hadi 851,563 kwa mwaka 2021. Ardhi ya malisho na ushoroba wa wanyamapori umepungua kwa 44.6% katika hifadhi hali ambayo inachochea kuongezeka kwa mkaribiano na migogoro ya binadamu na wanyamapori na magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa binadamu. 

Pia alibainisha kuzorota kwa mazingira na mfumo wa ikolojia kutokana na uwiano usio endelevu kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu na mifugo na kuongeza mkaribiano na wanyamapori katika eneo hili la urithi wa Dunia wa UNESCO. Alieleza zaidi kuwa, kwa vile NCA ni ardhi iliyotengwa kwa mujibu wa sheria (Reserved Land), hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na usambazaji wa maji ya bomba na miundombinu ya umeme. Kwa hiyo, upatikanaji wa huduma za kimsingi za kijamii kama vile ardhi, vyanzo mbadala vya mapato, huduma ya maji safi na salama, elimu na huduma za afya kwa wakazi waliopo eneo hilo ni mgumu. Kwa mfano, kufikia mwaka wa 2017, ilikadiriwa kuwa kiwango cha kutojua kusoma na kuandika kilikuwa 64%, na katika 80% ya wakazi wote wa NCA walikuwa wanamiliki 3% tu ya mifugo. Hii ikimaanisha kuwa 97% ya mifugo yote iliyopo eneo la hifadhi inamilikiwa na watu wanaoishi nje ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro.

Prof.Malebo alifahamisha kuwa, ni wakati wa mapitio shirikishi ya Mfumo wa Matumizi ya Mseto ya Ardhi (MLUM) wakazi waliifahamisha Serikali juu ya mahitaji yao ikiwa ni pamoja na kupata mahitaji na huduma muhimu za kijamii ambazo haziwezi kutolewa katika NCA ili kukabiliana na changamoto hizo, wakazi na washikadau walipendekeza kuwepo na Mpango wa Kuhama kwa Hiari kutoka eneo la Hifadhi. Kwa hivyo, Serikali inaunga mkono Mpango wa kuhama kwa Hiari ulioasisiwa na wananchi wenyewe ukihusisha mawazo na mapendekezo ambayo yalitoka kwa wakazi wa NCA. Prof. Malebo pia alibainisha kuwa, huduma za kijamii katika NCA bado zinaendelea kutolewa na zinafanya kazi ambazo zinajumuisha shule za msingi 29, shule za sekondari 3, zahanati 12, vituo vya afya 2 na hospitali 1. Serikali imeendelea kutoa huduma ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa NCA ambapo jumla ya wanafunzi 1,836 wanasaidiwa kwa gharama ya TZS 1.8 bilioni kwa mwaka (USD 769,885.16).

Hata hivyo, Prof. Malebo alitahadharisha kuwa, bado kuna haja ya kuongeza huduma kutokana na idadi ya watu inayoendelea kuongezeka kwa kasi hali inayovuka uwezo wa kuwahudumia hivyo Serikali inaendelea kuwaelimisha wakazi waliosalia NCA kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na masuala mahususi ya wafugaji na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), bomba litakalosafirisha mafuta yanayozalishwa kutoka maeneo ya Ziwa Albert nchini Uganda hadi bandari ya Tanga, Prof. Malebo alikiambia kikao hicho kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahitaji kumjulisha Mwandishi na jumuiya ya kimataifa kuwa, sio tu Wamaasai, Akie, Barbaig na Wataturu wanaishi katika njia ya bomba la mafuta, bali kuna makabila 31 kwa jumla. Serikali inasisitiza msimamo wake kwamba, makabila yote ya Tanzania yana haki sawa mbele ya sheria na hakuna kabila lolote lenye haki na kupewa kipaumbele zaidi ya mengine. Prof. Malebo alisisitiza kuwa, wakati wa usanifu, Serikali ilihakikisha kuwa inazingatia kanuni ya Kupata Ridhaa Huru, Kabla na Kwa Kutaarifiwa (FPIC) ambapo mazungumzo na Makubaliano yametiwa saini na jamii zote zinazohusika katika eneo linapopita bomba hilo. Zaidi ya hayo, mradi wa EACOP unaelimisha na kushughulikia masuala yote ambayo yameelezwa na jamii kwa namna ambayo ni sahihi kitamaduni na kwa kuheshimu taratibu kwa viwango vya Kitaifa na Kimataifa vya haki za binadamu. Zaidi ya hayo, utaratibu wa Ufuatiliaji na Utekelezaji wa EACOP unahusisha kushirikisha katika ngazi ya jamii kwa kutumia mbinu za kitamaduni ili kufuatilia utekelezaji na kupata maoni ya jamii katika hatua za utekelezaji wa mradi.

Amesema kuna utaratibu madhubuti wa ufuatiliaji wa masuala na kero zinazotolewa na jamii ambako bomba hilo linapita.

Profesa Malebo alisisitiza kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongozwa na misingi ya utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu. Aidha alisisitiza kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa uhamaji wowote wa wananchi toka eneo moja hadi lingine unafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi ili kuhakikisha haki na maisha ya ufugaji yanaheshimiwa na vile vile uharibifu wa mazingira ya hifadhi unapungua na kudhibitiwa.

Wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho ni Bi. Nkasori Milika Sarakikya, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Daniel Loiruck, Afisa Tawala kutoka mkoa wa Arusha, Bi.Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi na Bi. Prisca Kasalama, Afisa Msaidizi wa Kamati ya 3 ya Masuala ya Watu wa Asili, wote kutoka Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani.
 

No comments