SERIKALI YASAINI MKATABA WA UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI
Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa Daraja la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na barabara za maungio zenye urefu wa mita 700 katika barabara ya Fire - Ubungo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 97.1 ambapo kazi ya ujenzi itatekelezwa kwa miezi 24.
Mkataba huo umesainiwa leo Oktoba 22, 2024 Mkoani Dar es Salaam kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS) na Mkandarasi wa Kampuni ya China Communications Construction Company Limited na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na viongozi wengine.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaondoa kero kwa wananchi na adha ya usafiri kutokana na eneo hilo kujaa maji mara kwa mara na kusababisha barabara kufungwa na kutopitika mvua zinaponyesha.
Bashungwa amemuelekeza Mkandarasi huyo kukamilisha maandalizi na kupeleka vifaa na mitambo ndani ya miezi mitatu katika eneo la Jangwani ili kazi iweze kuanza na kuhakikisha anajenga haraka kwa mujibu wa usanifu na mkataba kama ilivyopangwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaenda sambamba na ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi ambao utatekelezwa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ikiwa ni katika programu ya uendelezaji wa Bonde la Msimbazi.
Bashungwa amebainisha kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi Bilioni 125 kwa ajili ya kurejesha miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam iliyoathiriwa na mvua za El-Nino ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la Kigogo, daraja la Mpiji chini, daraja la Mtongani, daraja la Mkwajuni, daraja la Mzinga, daraja la Nguva na box kalavati la Mikadi, daraja la JKT – Ununio, daraja la Kisarawe, Amani, Gomvu, Geti jeusi, mifereji ya maji Kigamboni – Kibada na maeneo mengine.
Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa mkandarasi aliyeshinda zabuni ya ujenzi ni kampuni ya China Communications Construction Company Limited na kusimamiwa na kampuni ya Leporogo Specialist Engineers ya Afrika Kusini ikishirikiana na Afrisa Consulting Ltd ya Tanzania na Dong Myeong Engineering Consultants & Architecture Co. Ltd ya Korea Kusini.
Naye, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Hassan Zungu ameeleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa daraja la Jangwani ni matokeo ya 4R za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka historia ya kuanza kutekeleza ujenzi wa daraja la Jangwani.
Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Jangwani ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Dar es Salaam kwa kuboresha barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Usafiri.
No comments