Breaking News

NAIBU WAZIRI KIGAHE: AHIMIZA URASIMISHWAJI WA BIASHARA

Naibu waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Exaud Kigahe amehimiza urasimishwaji wa biashara ndogo za kati na kubwa ili kuongeza ufanisi wa ukuaji wa uchumi kupitia kodi zinazotokana na wafanyabiashara Nchini Tanzania.

Akizungumza Jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa pili uliowakutanisha wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) na wadau wake lengo ni kujadili fursa, mafanikio pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ha biashara hususani katika eneo la Sajili na Leseni za Biashara ambapo BRELA ndiyo lango la uanzishaji wa biashara nchini.

Amesema BRELA inajukumu kubwa la kurasimisha biashara huku lengo la serikali kupitia wizara hiyo ni kuhakikisha biashara hizo zinaleta uhimilivu toshelezi wa uchumi ili fedha zinazopatikana kutokana na kodi hizo zielekezwe katika utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati.

"Ukuaji wa biashara na uchumi nchini unaendelea kuimarika na kuweza kufikia malengo ya Serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Tanzania wa kufikia uchumi wa kati na endelevu ifikapo mwaka 2025". Alisema Kigahe.
Alisema BRELA haiwezi kufanikiwa kutekeleza majukumu yake ikiwa peke yake,inategema ushirikiano wa karibu na Sekta za Umma na Sekta Binafsi. Ndiyo maana Mkutano huu ni muhimu sana kufanyika ili kufanya tathmini ya wapi BRELA imetoka, ilipo sasa na wapi inaelekea kwa zikizingatia nafasi yake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa. 

"Matarajio yangu Mkutano huu utakuwa nyenzo muhimu katika kuifanya BRELA kuwa taasisi bora na ya mfano katika kutoa huduma bora za sajili na leseni, kutoa elimu kwa jamii ya wafanyabiashara na wawekezaji ili uwekezaji na biashara zinazofanyika ziwe na tija, faida ipatikane kwa wafanyabiashara na Serikali ikusanye kodi kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na uchumi wa nchi uweze kukua na kuimarika". Alisema Mhe. Kigahe

Katika hatua nyingine Kigahe amevutiwa na Kauli Mbiu ya Mkutano wa Mwaka huu ‘Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini’ (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation) ambayo inatasaidia Mifumo ya Kitaasisi kusomana kwa lengo la kutoa kero zisizo za msingi kwa Sekta Binafsi kwani Serikali ilishatoa maelekezo kwamba ifikapo Mwezi Desemba, 2024, Taasisi za Serikali ziwe na mifumo inayosoamana.
"Nafahamu tangu mwaka 2018 BRELA imekuwa ikitoa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao (Online Registration System) na (Tanzania National Business Portal) Mifumo hii imepunguza muda, gharama kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara". Alisema Mhe. Kigahe

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa viwanda na Biashara, Mwenyekiti wa bodi BRELA, Profesa Neema Mori amesema kupitia kauli mbiu ya “Mifumo ya kitaasisi inayosomana na uwezeshaji wa biashara nchini” hivyo basi watahakikisha mifumo yote inasomana ili huduma ziweze kuwafikia wadau

“Kabla ya mifumo hii kuanza wateja walikuwa wanalazimika kutoka sehemu zote za nchi kuja kupata huduma Dar es Salaam. Huduma nyingine zilikuwa zinagharimu kiasi cha TZS 1,000 lakini wateja walilazimika kutoka Mbeya, Arusha, Mwanza, Rukwa na mikoa mengine kufuata huduma hii.

“Mfumo huu wa ORS umetimiza miaka sita sasa, ni dhairi teknolojia na baadhi ya sheria zimebadilika sana. Hivyo, sisi kama BRELA tulishaanza maboresho ya Mfumo huo kwa kuufanya uwe bora na rafiki zaidi na katika mfumo wa sasa kuna baadhi ya taarifa zinazolazimu kujazwa zaidi ya mara moja, kitu ambacho mfumo ungeweza kuvuta taarifa hizo bila kuhitaji kujazwa tena.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu -BRELA, Godfrey Nyaisa amesema washiriki wa mkutano huu wa pili watajikita katika kujadili maswala mbalimbali huku maoni pamoja na changamoto zitakazoibuliwa zitatafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Alisema Mkutano wa mwaka huu jumla ya washiriki zaidi ya 350 na imebeba kauli mbiu ya "Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini




No comments