Breaking News

KILIMO BILA MBOLEA NI SAWA NA KUTWANGA MAJI KWENYE KINU - KIHENZILE

John Mongela Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara akiwa katika picha na Eliurd Mwaiteleke, Meneja wa Mipango, Taathmini na Ufuatiliaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakati wa Mkutano wa mabalozi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Mufindi Kusini tarehe 5 Oktoba 2024.

IRINGA
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb) amewapongeza wananchi wa Iringa kwa kuzingatia matumizi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.

Amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano maalum wa wadau wa kilimo na mazingira, Jimbo la Mufindi Kusini uliolenga pia kuhamasisha ushiriki wa wananchi hao kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Novemba, 2024. 

Amewataka kuongeza maarifa katika matumizi ya mbolea kupitia elimu inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupitia kampeni ya “Kilimo ni Mbolea” yenye kauli mbiu “Ongeza Mavuno kwa Matumizi Sahihi ya Mbolea” inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini. 

"Kilimo ni uti wa mgongo, kilimo bila mbolea ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu, Hongereni wana Mufindi mnaziishi ahadi za Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo, endeleeni kuijenga Nchi yetu."

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA), Meneja wa Sehemu ya Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji, Bw. Eliurd Mwaiteleke amesema, Mamlaka inaendelea na kampeni ya kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa lengo la kuongeza hamasa ya matumizi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha usalama wa chakula kwa familia na taifa kwa ujumla.

Amesema Mamlaka imeamua kuwafikia wakulima wa Iringa kwa lengo la kuwakumbusha wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbolea katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuhamasisha kuendelea kujitokeza ili kuhuhisha na kujisajili katika mfumo wa ruzuku ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku.

Ameeleza umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea kwa kipindi hiki kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu kunakohitaji ongezeko la uzalishaji wa chakula ili kukidhi mahitaji,
ili, ukuaji wa miji, ongezeko la ujenzi wa miundombinu na huduma nyingine za kijamii unapunguza eneo linalofaa kwa kilimo na 

Mwisho ni uwepo wa hamasa ya utunzaji wa mazingira ili kuepuka ukataji holela wa miti kwa ajili ya kuanzisha mashamba mapya na hivyo kulazimu kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbolea.   

Akitoa elimu ya mbolea katika mkutano huo Afisa Udhibiti Ubora wa TFRA, Stephano Chimile alieleza Kanuni kuu nne za kuzingatia kwenye matumizi ya mbolea kuwa ni pamoja na kutumia Mbolea sahihi, kutumia kiwango sahihi, kuweka mbolea muda sahihi na mwisho ni kuweka eneo sahihi la mmea na kueleza kanuni hizo zikizingatiwa mavuno ni dhahiri. 

Aidha, wajumbe walikumbushwa ili kufanikiwa wanapaswa kupima afya ya udongo ili kujua mahitaji ya udongo wanaoulima.


Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposa Kihenzile ( Mb) (katikati) akiwa katika picha na Meneja wa Sehemu ya Mipango, Taathmini na Ufuatiliaji wa TFRA Eliurd Mwaiteleke  

No comments