Breaking News

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM DAR WATOA ELIMU KWA WAGANGA TIBA MBADALA JUU YA ATHARI ZA LAMRI CHONGANISHI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linaendelea kusimamia mikakati ya kuhakikisha usalama wa Jiji la Dar es Salaam unakuwa wa hali juu ikiwa ni pamoja na kuyashughulikia kwa mujibu wa sheria  matukio ya kikatili dhidi ya watoto na wanawake yanayohusisha vitendo vya kulawiti na kubaka ambavyo wakati mwingine yanapelekea wahanga kupoteza maisha.

Katika hatua hiyo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam tarehe 03 Septemba, 2024 limefanya kikao na waganga wanaojulikana kama wa tiba mbadala 80 kwa lengo la kuwaelemisha kuacha kujihusisha au kufanya ramli chonganishi ikiwa na pamoja kuacha tabia ya kuwapa masharti baadhi ya wateja wao kuwa ili wafanikiwe kwenye biashara na kupata utajiri lazima wafanye vitendo viovu vya  kuwalawiti au kuwabaka watoto wadogo .Katika hili Jeshi limetoa tahadhari na kuwaonya vikali watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Wakati huo huo, Jeshi Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam katika kusimamia mifumo ya kisheria na utekelezaji wa taarifa ya tume ya haki jinai, Jeshi limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya kihalifu ambao baadhi yao  wamepatikana na hatia na kuhukumiwa kwa  kupewa adhabu. 

Jeshi la Polisi limekuwa likichukizwa sana na vitendo vya Ubakaji na ulawiti na katika hatua hiyo washtakiwa katika kesi 16 kuanzia za makosa ya kubaka na kulawiti zilizo sikilizwa kati ya Julai hadi Agosti 2024 walihukumiwa adhabu za vifungo akiwemo Boniphace Paul @ devi (24) mkazi wa Mbezi kwa Msuguli, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, shauri la jinai No. 192/2023 mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza kwa kosa la kumbaka na kulawiti mwanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 13 ambapo baada ya shauri lake kusikilizwa tarehe 15/08/2024 mshtakiwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa na kufungwa kifungo cha maisha jela.

Mshtakiwa George Godfrey (21) Mkazi wa Chanika alimakatwa maeneo ya Coco beach na kufikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa kosa la Unyang’anyi wa Kutumia Silaha ambapo baada ya shauri lake kusikilizwa tarehe 28/08/2024 alipatikana na hatia na kuhukumiwa na kufungwa kifungo cha miaka 30 jela.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi tarehe 03/ 09/ 2024 majira ya saa mbili (2) usiku, lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa maeneo ya Kawe Tanganyika Pekers kulikuwa na watu wawili waliokuwa na mapanga huku wakitishia na wanawapora wapita njia.

Ufuatiliaji wa Polisi ulifanyika haraka na kuwakuta watu hao,  walipotaka kukakamtwa walikakaidi na kutoa mapanga kutaka kumdhuru mmoja wa askari, ambaye  alijihami kwa kupiga risasi hewani na baadae alipokuwa kwenye hatari kubwa ya kudhuriwa  alimjeruhi kwa risasi mtuhumiwa mmoja Festo Maricha  (27) mkurya, Mkazi wa Mbezi Luis na mwenzake ambaye hakufahamika jina alikimbia. Mtuhumiwa amepelekwa Hospitali ya Mwanayamala kwa matibabu. 
  
Jeshi lal Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali zitazosaidia mkakati wa kuzuia zaidi vitendo vya kihalifu  ili Jiji la Dar es Salaam liendelee kuwa salama.


Imetolewa na;
Muliro J. MULIRO - SACP
Kamanda Kanda Maalum ya Polisi 
Dar es Salaam

No comments