Breaking News

WAZIRI MAVUNDE AFAFANUA KUHUSU VISION 2023

Itakumbukwa kuwa, nchi yetu imefanya utafiti wa kina (High Resolution Airbonrne Geophysical Survey) kwa asilimia 16, pamoja na kufanya kwa kiasi hicho Sekta ya Madini imekuwa na mafanikio yafuatayo.

Kuhusu Madini ni Maisha na Utajiri

# Kwa Mwaka wa fedha uliopita (2022/2023) imekuwa ya kwanza kwa kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia 56 ya fedha zote za kigeni zilizoingia hapa nchini; mauzo ya bidhaa nje ya nchi yalikuwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 3.1; 

# Mapato ya kodi ya ndani yaliyokusanywa yalikuwa ni shilingi trilioni 2.1 sawa na asilimia 15 ya mapato yote ya ndani; 

# Mzunguko wa fedha (transaction) uliokuwepo kwenye vituo vya ununuzi 100 na masoko 42 yalikuwa ni shilingi trilioni 1 na bilioni 700; 

# Maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yalikuwa ni shilingi bilioni 678; fedha iliyotumika kwenye manunuzi ya bidhaa na usambazaji wa huduma (local content) ni shilingi trilioni 3.1. 

# Sasa unajiuliza tukifanya huu utafiti wa kina kwa angalau mara mbili au tatu ya huo wa asilimia 16 tuliokwishafanya mpaka sasa hali itakuwaje, na hapo ndio ikazaliwa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri.

# Madini ni Maisha kwasababu kupitia utafiti huo wa kina tunaenda kuunganisha sekta zingine, zikiwemo za kilimo, maji na afya, kupitia utafiti huu, tutaweza kuonesha vyanzo vikubwa vya maji, wenzetu wa kilimo wana mkakati wa utekelezaji wa mabonde 22 nchini kote na ujenzi wa mabwawa 100 kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji sisi tunaweza kuwaonesha ni wapi kuna vyanzo vya maji. 

# Maeneo mengi nchini yameathiriwa na tindikali na njia pekee ya kutibu ni kupitia madini ya chokaa ya kilimo, Zaidi ya hekta milioni 3.7 ya Tanzania imeathiriwa na chumvi na njia pekee ya kutibu hilo ni kutumia madini ya jasi (gypsum).

# Ukienda Rukwa na Songwe tumegundua kuwa gesi ya helium ambayo bado tunaendelea kufanya utafiti inawezekana ukiondoa Urusi na Marekani, Tanzania ikaingia kwenye ramani ya dunia kwa kuwa na hifadhi kubwa ya gesi hiyo inayotumika kuendeshea mashine ya MRI.

● Hivi sasa tunatumia fedha nyingi sana kuagiza mbolea nje ya nchi, mbolea tunazoagiza sana nje ya nchi ni mbolea ya kupandia na kukuzia (DIP na Urea) ambapo mbolea ya urea inatengenezwa kupitia makaa ya mawe ambayo sisi tunayo kwa wingi tuna hifadhi kubwa Kiwira na maeneo mengine.

● Kwahiyo baada ya kumalizika kwa utafiti wetu wa kina  tuna uwezo wa kuwaleta wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza hapa kwa kuwa tuna mali ghafi ya kutosha na mkulima wa tanzania ataweza kupata mbolea hapa kuliko kuagiza kama sasa.

● Hiyo ni kinadharia, sasa kivitendo baada ya wasilisho kuhusu azma hiyo, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuongezea bajeti Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 mwaka wa fedha uliopita (2023/24) mpaka shilingi billioni 231 mwaka huu wa fedha (2024/25).

● Kati ya fedha hizo, zaidi ya bilioni 115 zinaenda katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambazo zitatumika kujenga maabara mbili za kikanda Geita na Chunya kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji kupata taarifa sahihi za sampuli ambazo wanazipeleka lakini pia itajengwa maabara kubwa ya kisasa Dodoma (State Art Laboratory) na tumefungua mashirikiano mazuri na GTK ambayo ni taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini ya Finland kwa ajili ya kuwaandaa watu wetu ili maabara hizo zitakapokamilika tuwe na wataalamu tayari.
# Pia, tunanunua Helkopta na kuifunga vifaa maalum kwa ajili ya kufanya huo utafiti wa kina ili kuwaondolea wachimbaji wadogo adha ya kuchimba kwa kubahatisha, Sekta ya Madini hakuna uchawi bali ni Sayansi, utajiri wetu ni taarifa sahihi za miamba za maeneo madini yalipo.

Kuhusu Madini Mkakati

# Kwenye madini mkakati mfano, Dunia hivi sasa inahama kutoka kwenye matumizi ya Diesel na Petrol kwenye magari kwenda kwenye magari ya umeme kwa ajili ya kupunguza matumizi ya hewa chafu, kwenye betri ya magari ya umeme moja kati ya malighafi inayohitajika sana ni madini ya kinywe (Graphite) ambayo mahitaji yake hivi sasa ni tani milioni 6.5 na uzalishaji wa dunia ni tani milioni 1.2 China ikiongoza kwa kuwa na asilimia 64 ya uzalshaji wote wa kinywe duniani, 

# Kwa Afrika, Madagascar inaongoza kwa kuzalisha asilimia 13 ya uzalishaji wote duniani wa pili akiwa ni Msumbiji akizalisha asilimia 10 na Tanzania ikiwa ya tatu kwa kuzalisha asilimia 0.64 na huyo ni Mtanzania mmoja tu anaitwa God Mwanga pale Handeni na tuna leseni 9 za uchimbaji mkubwa wa madini hayo ambayo yote yakianza uzalishaji tutapiga hatua kubwa sana.

Kuhusu Eneo la Mirerani na Madini ya Tanzanite

# Eneo la Mirerani ni eneo tengefu na lilitungiwa Kanuni kwamba biashara ya madini ya tanzanite inapaswa kufanyika pale Mirerani, na kiasi cha shilingi bilioni 5 zilitengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Biashara ya Madini ya Tanzanite pale Mirerani (Tanzanite Exchange Center – TEC) na ujenzi wake umefikia asilimia 84 na kitakamilika muda sio mrefu. Hivyo, biashara yeyote ya Tanzanite kabla ya kutoka nje ya eneo la Mirerani itafanyika ndani ya kituo hicho.

# Katika mikakati ya kuilinda Tanzanite, kwanza Bunge la Mwezi wa 9, tunaenda kufanya Mabadiliko ya Sheria ili kuruhusu Maonyesho ya Kimataifa na Minada ya ndani na kimataifa ili tuendelea kuchochea biashara ya tanzanite pamoja na kuitangaza duniani.

# Mathalan, Mwaka wa Fedha 2014/2015, Wizara ilikusanya shilingi bilioni 168 lakini nashukuru watangulizi wangu baada ya kufanya mabadiliko ya kisheria hivi sasa kuanzia Mwezi Julai, 2023 hadi tarehe 30 Juni, 2024, tumekusanya Shilingi bilioni 753 na kwa Mwaka huu (2024/25) tumepangiwa kukusanya shilingi trilioni 1 unaweza kuona jinsi Sekta hii inavyokuwa kila mwaka.

No comments