Breaking News

MUHIMBILI KIDEDEA KWA TAASISI ZAHUDUMA ZA AFYA SABASABA

Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila imepata tuzo ya mshindi wa kwanza katika kundi la watoa huduma za afya katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu sabasaba.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa hospitali leo na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akifunga rasmi maonesho hayo yaliyofanyika kwa takribani siku 16 kwa kuhusisha mashirika, taasisi za ndani na nje ya nchi.

Tuzo hiyo imetokana na ubora na utendaji kazi wa wataalam wake waliokuwa wakitoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ambapo wananchi walipata fursa ya kupata elimu, ushauri, uchunguzi na matibabu ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma.
Aidha,wananchi waliotembelea banda la hospitali hiyo wameishukuru na kuipongeza Muhimbili kwa kuwasogezea huduma katika kipindiki hiki cha sabasaba kwani wamenufaika na huduma za mbalimbali zilizokuwa zikipatikana katika banda hilo.

Kwa upande wa watumishi waliokuwa wakitoa huduma katika banda hilo wamesema wanatambua ni kwa kiasi gani Watanzania wana matarajio makubwa na Muhimbili, hivyo siku zote watafanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma bora kwa weledi mkubwa na kwa wakati unaostahili kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani.

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi Julai 3, 2024 na Rais wa Msumbiji Mheshimiwa Filipe Jacinto Nyusi ambaye aliambatana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan

No comments