Breaking News

KAMATI YA BUNGE YA PAC YAPIGWA MSASA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameipongeza kamati ya kudumu ya  Bunge ya Hesabu za serikali (PAC) kwa kusimamia na kushauri vema mashirika yanayotekeleza miradi mbalimbali ya serikali, kwani wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwenye mafanikio ya miradi hiyo.

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akifungua semina ya kamati ya Bunge ya PAC iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wakati wakiwasilisha mpango wa bajeti ya miradi ya maendeleo itakayotekelezwa na TPDC kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Dkt. Biteko alisema kupitia bajeti hiyo TPDC itatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo uchorongaji wa visima vya kutafuta gesi eneo la Mnazi Bay pamoja na kumtafuta mbia kwa ajili ya kushirikiana nae kwenye kazi hiyo pamoja na kukamilisha tafsiri ya taarifa za mitetemo kwenye kitalu cha Eyasi-wembere.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Kamati ya PAC Mhe. Japhet Hassunga (Mb.) ameitaka TPDC kuangalia uwezekano wa kuwekeza mtaji  wa kutosha kwenye miradi ya gesi badala ya kutegemea wafadhili pekee na kutolea mfano nchi ya Misri ambapo uwekezaji wa Suez  Canal ulifanikishwa na wananchi wa Misri kwa kutoa fedha za uwekezaji na kufanikiwa kwenye mradi huo,hivyo ni vema kuiga kutoka kwa wenzetu ili kufanikiwa. 

Amesema nchi  nyingi duniani zenye utajiri wa gesi na mafuta zimeendelea sana na kwa kuwa Tanzania inayo gesi ya kutosha, hatupaswi kuendelea kuwa maskini hivyo ameitaka TPDC kuwekeza kwenye uchorongaji na taarifa za upatikanaji wa rasilimali hizo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio ameihakikishia Kamati kuwa Wizara itaendelea kusimamia miradi ya kimkakati  inayotekelezwa na taasisi zake hususani ile ya kusambaza gesi kwani iko kwenye mkakati wa Serikali na kwenye dira ya maendeleo ya Serikali.

Ameitaka TPDC kuishirikisha Sekta binafsi kwenye utekelezaji wa fmiradi yake kwani TPDC pekee haiwezi kufanikisha na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati.