Breaking News

REA NA JESHI LA MAGEREZA WAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA KUHUSU MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi Hassan Saidy (Kushoto) akiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee Nyamka (Kulia) wakishikana mikono mara baada ya kusaini Hati ya Makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya ujenzi wa miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia Magerezani, Leo Tarehe 9 Aprili, 2024 katika ukumbi wa makao makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi Hassan Saidy (Kushoto) akiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee Nyamka (Kulia) wakisaini Hati ya Makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya ujenzi wa miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia Magerezani, Leo Tarehe 9 Aprili, 2024 katika ukumbi wa makao makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi Hassan Saidy akihutubia wakati wa hafla hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Magereza makao makuu, Jijini Dodoma
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee Nyamka akihutubia wakati wa hafla hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Magereza makao makuu, Jijini Dodoma
Menejimenti na Watumishi wa REA wakiwa pamoja na Viongozi Wakuu wa Taasisi hizo mbili kwenye picha ya pamoja mara baada ya kukamilika kwa hafla hiyo, Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu akihutubia wakati wa hafla hiyo katika ukumbi wa Jeshi la Magereza, Jijini Dodoma, leo Tarehe 9 Aprili, 2024.
Askari kutoka Jeshi la Magereza makao makuu wakifuatilia hotuba za Viongozi wakati wa hafla hiyo katika ukumbi wa Jeshi hilo, Jijini Dodoma, leo Tarehe 9 Aprili, 2024.
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakifuatilia hotuba za Viongozi wakati wa hafla hiyo katika ukumbi wa Jeshi la Magereza, Jijini Dodoma, leo Tarehe 9 Aprili, 2024.
Askari kutoka Jeshi la Magereza makao makuu wakiwa pamoja na Menejimenti ya REA wakiwa pamoja na Viongozi Wakuu wa Taasisi hizo mbili kwenye picha ya pamoja mara baada ya kukamilika kwa hafla hiyo, Jijini Dodoma.

Dodoma:
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee Nyamka, leo tarehe 9 Aprili, 2024 wamesaini Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) ya Utekelezaji wa Programu ya Ujenzi wa Miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye magereza 129 Tanzania Bara.

Katika utekelezaji wa Makubaliano hayo, REA italiwezesha Jeshi la Magereza katika Ujenzi wa Mifumo 126 ya Gesi Vunde (Biogas), Usimikaji wa Mifumo ya 56 ya Gesi ya Kimiminika (LPG), Uboreshaji wa Mfumo wa Gesi Asili katika Gereza Lilungu – Mtwara, Ununuzi wa tani 1,147 za mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) na majiko 412, pamoja na Ununuzi wa Mashine 61 za kutengeneza Mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya mazao (Charcoal Briquettes).

Aidha, REA na Magereza zitashirikiana pia katika Usimikaji wa Mfumo wa Matumizi ya Gesi Asili katika Kaya 93 eneo la Gereza Keko, Kaya 548 katika Eneo la Ukonga Complex na majiko nane (8) ya Biashara eneo la Ukonga pamoja na utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi 280 wa Jeshi la Magereza kuhusu uendeshaji wa miradi ya nishati safi.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 1 Novemba, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo kwa Taasisi zote za Umma ambazo zinatumia nishati isiyo safi wakati wa kupika chakula cha watu wasiopungua 100, kuacha matumizi ya nishati chafu kwa ajili ya utunzaji wa mazingira pamoja na afya za watu.

Awali katika hotuba yake, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Kizito Jaka, amesema Jeshi la Magereza lina jumla ya Magereza 129 katika mikoa yote Tanzania Bara ambayo yanahifadhi wastani wa wafungwa na mahabusu 32,000 kwa siku. 

Ameongeza kuwa vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia chakula cha wafungwa na mahabusu ni kuni kwa asilimia 98, mkaa mbadala kwa asilimia 0.9 na gesi asilia ni kwa asilimia 1.1. 

“Mahitaji ya kuni kwa ajili ya kuandaa chakula cha wafungwa na mahabusu magerezani ni mita za ujazo 69,017.5 kwa mwaka. Kuni hizi hupatikana kutoka kwenye Misitu ya asili iliyopo katika maeneo ya Magereza, Misitu ya kupandwa, matawi ya Miti yanayopunguzwa katika maeneo mbalimbali na zingine hununuliwa.” Amekaririwa Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Kizito Jaka.

Naye Mhandisi Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuwa taasisi ya kwanza ya umma kuanza safari ya mabadiliko ya kuacha matumizi ya nishati chafu na kuanza kutumia nishati safi kivitendo.

“Sisi kama Wakala wa Nishati Vijijini, tuliwasiliana na Taasisi tofauti za Umma lakini kwa upande wa Jeshi la Magereza walitoa kipaumbe suala la nishati safi, na leo hii, Magereza imekuwa Taasisi ya kwanza kusaini Hati ya Makubaliano ya kuanza safari ya matumizi ya nishati safi.” Amekaririwa Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi, Saidy.

Mhandisi Saidy ameongeza kuwa REA pia ilikuja na wazo la kuwahamasisha Viongozi, Maafisa na Watumishi 15,920 wa Jeshi la Magereza watasambaziwa mitungi ya gesi ya kilo 15 pamoja majiko ya gesi “LPG Starter Packs” ili kuwahamasisha kutumia nishati safi ya kupikia.

Mhandisi Saidy ametoa rai kwa Viongozi na Watumishi wa Jeshi la Magereza hata baada ya kuisha kwa gesi ya kuanzia, Watumishi hao waendelee kutumia gesi kama chanzo cha nishati safi ya kupikia majumbani.

Ninawaomba Viongozi ambao tupo hapa, tukawahimize Maaskari na Watumishi wengine wa Jeshi la Magereza kuanza kujenga utamaduni wa kutumia gesi, hatutaraji baada ya gesi ya kuanzia ya kilo 15 ikisha basi mitungi isije ikawekwa chini ya uvungu, hapana, matumizi yakawe endelevu.

Kwa upande wake Kamishina Jenerali wa Jeshi la Magereza Mzee Nyamka amesema, Programu ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Magerezani inalenga kulinda rasilimali za mazingira na kuboresha afya za wafungwa, watumishi na Jamii. 

“Program hii imehusisha vituo vyote vya Jeshi la Magereza Tanzania Bara ambapo kila kituo kitakuwa na chanzo kikuu na chanzo mbadala cha nishati safi ya kupikia.” Amekaririwa Kamishina Jenerali, Mzee Nyamka.

Nitumie fursa hii, kumpongeza na kumshukuru Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amir Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa maono yake chanya ya utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa afya za Wananchi. 

“Naishukuru Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Wakurugenzi na Menejimenti ya REA kwa kukubali kuanzisha mashirikiano yatakayowezesha ujenzi na matumizi sahihi ya miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Vituo vya Magereza.”

“Ninawahakikishia kuwa nitasimamia na kufuatilia matumizi ya fedha za ruzuku zitakazotolewa na REA katika kutekeleza program hii ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais sambamba na kufikia malengo kwa ufanisi na tija iliyokusudiwa.” Alisisitiza Kamishina Jenerali, Mzee Nyamka.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (Mst.) Jacob Kingu amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuwa mfano kwa Taasisi za Umma ambazo zimechangamkia fursa ya kuanza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kwa kuanza kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Nawapongeza na Jeshi la Magereza, ninyi mtakuwa kama shamba darasa la wengine kujifunza maarifa ya nishati safi ya kupikia, ninaamini mashine ambazo mtazipata kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala, mtazitumia ipasavyo kwa kuwa mna mashamba, misitu na vyanzo vingi vya malighafi kwa ajili ya utenengezaji wa mkaa mbadala, nina amini kuwa mtatengeneza mkaa wa kutosha kwa ajili ya matumizi yenu na wa ziada kwa ajili ya kuuza.” Amekaririwa, Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Kingu.