Breaking News

NGORONGORO YAZINDUA ZOEZI LA UPIGAJI KURA KUWANIA TUZO YA KIVUTIO BORA

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imezindua zoezi la upigaji kura kuwania tuzo ya kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024 katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mamlaka hiyo mkoani Arusha.

Akizindua kampeni hiyo ya upigaji kura Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bi. Victorian Shayo amesema zoezi hilo litachukua siku 131 na litakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Amesema Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mwaka jana ilifanikiwa kushinda tuzo hiyo inayoandaliwa na World travel Awards inayojihusisha na kutoa tuzo mbalimbali na kuchochea kasi ya ukuaji wa utalii duniani.

Kaimu Kamishna huyo amesema tuzo hizo zina umuhimu mkubwa katika kuendeleza sekta ya Utalii duniani na kutoa wito kwa watanzania na wageni wote wanaotembelea nchini kupiga kura kwa wingi ili kuiwezesha Ngorongoro kutetea taji lake.

Akizungumzia kuhusu ongezeko la watalii nchini Bi. Shayo amesema mpaka kufikia nusu mwaka wa fedha wa 2023/24 hifadhi ya Ngorongoro imeshaingiza watalii zaidi ya laki tano ambapo wageni hao wameweza kuiwezesha Mamlaka kupata zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni mia mbili.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Utalii Bi. Mariam Kobelo ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii na kupata elimu kuhusiana na vivutio hivyo.

Naye Afisa Utalii Mkuu Bw. Peter Makutian amewapongeza wageni wote waliotembela Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kupiga kura kwa wingi na kuiwezesha Hifadhi hiyo kuwa kivutio bora barani Afrika kwa mwaka 2023.

Nchi tano zinawania tuzo hiyo ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini, Botswana, Misri na Malawi.