Breaking News

CUF WATUMA SALAM ZA POLE NA RAMBIRAMBI YAJALI YA ARUSHA

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)

SALAMU ZA POLE NA RAMBIRAMBI KUFUATIA AJALI MBAYA ILIYOONDOA UHAI WA WATU WASIOPUNGUA 25 ARUSHA:

CUF- Chama Cha Wananchi kimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa juu ya ajali mbaya iliyohusisha lori na magari madogo matatu iliyotokea jioni ya jana huko Ngaramtoni Kibaoni, Arusha na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 25 (wakiwemo raia 7 wa kigeni), majeruhi zaidi ya 21 na hasara kubwa.

CUF- Chama Cha Wananchi kinawaombea marehemu wote mafikio Mema Peponi, kinawapa pole na kuwaombea majeruhi wote wapone haraka, na kuwapa pole na kuwaombea Subira njema wale wote walioguswa na ajali hii mbaya ikiwa ni pamoja na waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki.

CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya ndani kuongeza weledi na uwajibikaji katika kushughulikia masuala ya Usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kuzingatia masharti ya Kiusalama kwa safari za malori zenye kubeba mizigo mizito (Abnormal Wide Loads) kwenye barabara za magari madogo na mabasi ya abiria.

Badala ya askari wa Usalama barabarani kutumia Kitengo hicho kuwa ni neema ya kujipatia kipato kwa kupitia makosa(yakiwemo ya kubambikiza) ya madereva na makondakta, ni muda muafaka sasa wakafanya majukumu yanaendana na jina lao ili kuepusha ajali zisizolazimu na pia kupunguza ukubwa wa madhara (severity) pale ajali hizo zinapotokea. 

Aidha, tunatoa wito kwa wamiliki wa magari, madereva na watumiaji wengine wa barabara kutimiza wajibu wao katika kuimarisha Usalama barabarani. Hili ni jukumu la pamoja na la kila mmoja wetu.

HAKIKA SOTE NI WA MWENYEZI MUNGU NA KWAKE SOTE TUNAREJEA!

HAKI SAWA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Februari 25, 2024
 

No comments