Breaking News

BILIONI 16 KUTUMIKA KUPITISHA UMEME ARDHINI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Februari 20, 2024 amehitimisha ziara yake Wilaya ya Temeke katika Jimbo la Temeke kwa kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi mkubwa wa kupitisha umeme ardhini (Underground Cable) maeneo ya kurasini Wilaya ya Temeke
RC Chalamila amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika nyanja mbalimbali zinazogusa ustawi wa jamii ikiwemo nyanja ya nishati kwa kutoa kiasi hicho cha pesa ambapo ifikapo machi mradi utakuwa umekamilika hivyo wananchi wataondokana na kadhia ya kukatikakatika kwa umeme

Aidha RC Chalamila amesema cable inayowekwa ardhini inauwezo wa kupitisha umeme takribani megawati 100 ina urefu wa kilomita 6.8 ambayo ndio mwarobaini wa kukatika kwa umeme " uwekezaji huu ni wa pesa nyingi ni lazima tumshukuru Rais Dkt Samia" Alisistiza RC Chalamila

Vilevile RC Chalamila ametembelea miradi mingine ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuweka jiwe la msingi baadhi ya miradi ambapo kwa sehemu kubwa katika miradi yote aliyopitia ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.

Sambamba na hilo RC Chalamila amefanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Lumo Temeke ambapo amesikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia majawabu papo hapo.

Kesho Februari 21,2024 RC Chalamila anatarajia kuendelea na ziara yake ya kutembelea miradi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Wilaya ya Kinondoni.


No comments