Breaking News

WAZIRI ULEGA AZIPA MBINU BODI ZA LITA NA NARCO,ATOA MAAGIZO HAYA.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewaomba wajumbe wa bodi za Wakala wa Elimu na  Mafunzo ya Mifugo (Lita) pamoja na ya Kampuni ya Ranchi za Taifa ( Narco), kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo nchini.

Pia Waziri Ulega ameizitaka bodi hizo zikitekeleza majukumu yake ipasavyo hazitakuwa na changamoto kubwa kuhakikisha sekta ya mifugo inasonga mbele na kuinua uchumi.

Waziri Ulega amebainisha hayo leo wakati akizindua bodi hizo katika ofisi ndogo za wizara yake zilizopo jijini Dar es Salaam

Lita inajishughulisha na utoaji wa mafunzo bora ya muda mrefu na mfupi kuhusu ufugaji wa kisasa na huduma za ushauri kwa wafugaji, lakini pia inafanya tafiti maeneo mbalimbali ili kusukuma maendeleo ya sekta ya mifugo.

Narco yenyewe inaendesha na kuanzisha ranchi kubwa za kibiashara, kusambaza mbegu bora za mifugo sambamba na kuwawezesha wafugaji wadogo kuboresha mifugo yao ili kufuga kisasa zaidi.

Akianza na taasisi ya Lita, Ulega ameitaka kuandaa vijana kwa weledi na umahiri ili wakimaliza mafunzo yao, wajiajiri badala ya kutembea mitaani kuhangaika kusaka ajira.

Pia, amewataka Lita kuandaa vijana watakaokuwa tayari kupewa mitaji ili kujisimamia katika uzalishaji sambamba na kufanya kazi kwa ukaribu na Narco.

"Huu ndio uwe mtazamano wetu, kijana anapofundishwa pale Lita atambue akimaliza anakuwa mwajiri kwa vijana wengine.Hatutaki kufundisha watu ili waende kuhangaika bali waingie katika biashara ya mifugo na mazao yake, Lita mna wajibu huo," amesema na kuongeza;

"Pia, nataka muende mbele zaidi wakiwa vyuoni muandalie mkakati wa biashara ikiwemo kuwaunganisha na taasisi za kifedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuwapa mbinu za kutekeleza mkakati wa kibiashara.Msifanye mambo yale yale kwa njia zile kila wakati, hatutalisaidia Taifa.”

Ulega ameieleza bodi na menejimenti ya Lita kuhakikisha inatengeneza vijana walio tayari kufanya biashara ya mifugo na mazao yake, kuwatafutia fursa za kuwaunganisha ili kupata mitaji.

Kuhusu Narco, Ulega ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha baadhi ya vijana wanaohitimu mafunzo ya BBT (Jenga Kesho iliyo Bora- inayolenga kuwainua vijana) wanapanga katika vitalu ili kuzalisha, akisema jambo hilo linapaswa kufanyika haraka.

Waziri Ulega amemtaka Mwenyekiti wa bodi hiyo, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, na wajumbe wake kuhakikisha anaibadilisha Narco na kuwa taasisi kimbilio na kiongozi wa kuuza nyama ndani na nje ya nchi.

“Yaani ikiwezekana asilimia 80 mawazo yenu yawe katika uuzaji wa nyama nje ya nchi, tunataka kutoka tani 14,000 za kila mwaka hadi kufikia tani 50,000. Mwenyekiti (Simbakalia) nenda kaangalie vitalu ng'ombe wanaofugwa wakitoka wanapelekwa wapi?

"Nataka Narco ibadilike haiwezekani mtu anapewa kitalu, halafu hakiendelezi...hapana lazima muwe na viwango tunakupa kitalu ili ukafanye kitu fulani na kwa muda gani? Na tutaka kujua ng'ombe wako akitoka anaelekea wapi lengo ni viwanda vyetu vipate malighafi," amesema Ulega.

Amesema baadhi ya watu wanaomiliki vitalu vina chaka, akimtaka Simbakalia kwenda kuviondoa, badala yake wapewa watu wenye uwezo wa kuviendesha kwa ufanisi na Narco itakuwa na mwelekeo mzuri.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Lita, Dk Pius Mwambene amesema hiyo ni bodi ya nne tangu kuanzishwa kwa taaasisi hiyo na itafanya kazi kwa miaka mitatu. Amesema kampasi za Lita zipo katika kanda nane isipokuwa kanda ya magharibi.

"Pamoja na mambo mengine Lita inatoa huduma za ushauri kwa maofisa ugani na wadau mbalimbali. Pia tunafanya tafiti atamizi zinazosaidia kuboresha huduma za ushauri tunazozitoa,” amesema.

No comments