PROF NDALICHAKO ASHIRIKI KILELE CHA BONANZA LA AFYA LA WAAJIRI, AIPONGEZA ATE
ATE kwa kushirikiana na wadau wa kazi na Ajira, wamehitimisha kilele cha Bonanza la Afya la Waajiri kwa mwaka 2023 lililobeba ujumbe unaosema “Kuimarisha Afya ya Akili ili Kuongeza Tija Mahali pa Kazi.”
Mgeni Rasmi katika Bonanza hili alikuwa ni Waziri wa Nchi, OWM-KVAU, Mhe. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (MB) ambaye pamoja na mambo mengine amewapongeza ATE kwa kufanya Bonanza hili kwa mara ya pili na kuwataka Waajiri Nchini kuweka mifumo endelevu ambayo pamoja na kufanya kazi pia itawapa fursa ya kuimarisha afya zao ikiwemo kuweka programu za mazoezi
Akitoa salamu za Ukaribisho, Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba - Doran alibainisha kuwa jumla ya makampuni 150 yameshiriki Bonanza hili ambapo kati yao 50 wameshiriki michezo, 15 wameweka mabanda na kuonyesha biashara zao.
Bonanza hili limehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Herry Mkunda ambaye ameahidi kuendelea kushirikaina na wadau na Serikali katika kuhamasisha umuhimu wa Afya na usalama katika maeneo ya kazi ili kuleta tija.
Akizungumza kwa niaba ya Wadau walioshirikiana na ATE katika kuandaa Bonanza hili, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, pamoja na mambo mengine amesisitiza kwamba ni lazima Wadau washirikiane kulinda nguvu kazi katika maeneo yetu ya kazi dhidi ya hatari mbalimbali zinazoweza kuathiri Uzalishaji kwa kupelekea changamoto ya Afya ya Akili pamoja na kuingia katika hatari ya Magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Ofisi ya Afrika Mashariki, Bi. Noreen Toroka amesema kuwa ILO itaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali akiwemo ATE, TUCTA, OSHA, WCF, NSSF, PSSSF na Serikali kuunga mkono programu za kukuza Ajira sambamba na kuzingatia Usalama na Afya mahali pa Kazi.
Bonanza la leo lilianza asubuhi kwa Mazoezi ya Viungo(Aerobics) kwa washiriki wote na kufuatiwa na michezo mingine kama vile mpira wa miguu (Football), Mpira wa Pete (Netball), Mpira wa Kikapu, Kuvuta kamba, Kukimbia na ndimu kwenye kijiko, Kukimbia na Magunia, pamoja na kukimbia na glasi ya maji.
No comments