GST YAHITIMISHA WIKI YA MAAFA DUNIANI
Maadhimisho ya Wiki ya Maafa Duniani yamefikia kilele chake leo Oktoba 13, 2023 katika viwanja vya Stendi ya Zamani Mkoani Manyara ambapo zaidi ya wananchi 2500 wametembelea banda la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kupata elimu ya Majanga ya Asili ya jiolojia.
Akizungumza kwa niaba ya Mtedaji Mkuu wa GST, Meneja wa Sehemu ya Mapping Economic Geology na Mkuu wa Kitengo cha Majanga ya Asili ya Jiolojia Gabriel Mbogoni ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote wanaoishi katika maeneo yenye miinuko yenye mawe na majabali kuchukua tahadhali ya Majanga ya Asili hususan katika kipindi hiki kinachotarajiwa kutokea kwa mvua za Elnino.
Mbogoni amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na 2019, GST ina jukumu la kufanya Menejimenti ya Majanga ya Asili ya Jiolojia kwa lengo la kuhakikisha madhara yatokanayo na Majanga hayo yanapungua.
Mbogoni ameyataja baadhi ya Majanga ya Asili ya jioloia yakiwemo matetemeko ya ardhi, milipuko ya volkano, sunami, kutitia kwa ardhi na maporomoko ya ardhi ambapo amesema GST imeshiriki katika maonyesho hayo ili kutoa elimu ya namna ya kupunguza madhara na kuepuka maafa yanayoweza kusababishwa na Majanga ya Asili ya Jiolojia.
Maadhimisho ya Wiki ya Maafa Duniani 2023 yenye Kauli Mbiu isemayo "Imarisha Usawa kwa Uthabiti Endelevu" yamefanyika Mjini Babati katika Mkoa wa Manyara ambapo yameenda sambamba na Wiki ya Vijana pamoja na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
No comments