DIWANI PAZI AWATOA HOFU WAZAZI WA WATOTO WALIOHITIMU DARASA LA SABA
DIWANI wa Kata ya Buguruni, Busoro Pazi amewahakikishia wazazi wa wahitimu wa Darasa la saba katika shule za kata hiyo kwamba hawatapangiwa shule za mbali kwa ajili ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Pazi aliyasema wakati akihutubia halaiki ya wazazi, wakazi wa buguruni, walimu wa shule ya msingi Buguruni na wanafunzi hao katika mahafali ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni hapo jana.
“Niwahakikishieni kwamba serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan imetekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo na kujenga madarasa 18 kwa kiasi cha Sh 360 milioni” alisema Pazi
Aliongeza kwamba sanjari na kiasi hicho kutumika kujenga madara hayo ambayo kwa wastani wake kila moja limetumia Sh 20 milioni pia fedha hizo hizo Sh 20 milioni kwa darasa moja ni Pamoja na ununuaji wa dawati 20 kwa kila darasa sawa na madawati 360.
Katika muktadha huohuo Pazi alisema tayari Sh 370 milioni zitatumika kujenga shule nyingine ya sekondari katika mtaa wa mivinjeni uliopo katika ya Buguruni ambapo ujenzi wake utaanza katika mwaka wa fedha 2023/24.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ayoub Twahiri alimshukuru Diwani wa kata hiyo, Busoro Pazi, Mbunge wa jimbo la Segerea Bona Kaluwa na Rais Dk Samia kwakuwapatia fedha kwa ajili ya uboreshwaji wa miundombinu ya shule yao.
“Kwakuwa wanafunzi katika risala yao wameeleza changamoto za shule yetu, na mimi nina Imani na serikali kwamba haijawahi kutupungukia hivyo naamini kwamba itaendelea kutuunga mkono katika utatuzi wa changamoto za shule hii” alisema Twahir
Miongoni mwa changamoto za shule hiyo ni uhaba wa matundu ya vyoo ambapo serikali imejitahidi kujenga matundu ya choo 10 ya wanafunzi kwa kiasi cha Sh 20 milionini na matundu 5 ya wanafunzi wa awali na walimu kwa thamani ya Sh 15 milioni hadi sasa kuna uhaba wa matundu 42 ya vyoo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa shule hiyo, Alhaj Abd Zuberi shule hiyo ina uhaba wa matundu 42 ya vyoo na kuwaomba wadau wa maendeleo kuwasaidia katika utatuzi wa changamoto za shule hiyo.
“Hii shule haiwezi kuendelezwa na serikali pekee, bali nguvu za Pamoja na wahisani zinahitajika katika ukarabati wa miundombinu chakavu ya shule kwani ina zaidi ya wanafunzi 2000” alisema
Sanjari na ujenzi wa matundu hayo ya vyoo serikali imetumia Sh 34 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ambapo kwa busara ya Mwalimu mkuu aliomba darasa moja kuwa maktaba ya kisasa.
No comments