ATE WAKUTANA NA WADAU KUJADILI MASUALA YA UKIMWI MAHALA PA KAZI
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikaina na Shirika la Kazi Duniani (ILO) leo, Jumatano, tarehe 9 Agosti 2023, wameandaa Mkutano wa majadiliano wa Sekta Binafsi na Wadau kujadili Mchango wa Sekta Binafsi katika kuzuia Maambukizi ya UKIMWI katika maeneo ya Kazi kupita uhamasishaji wa umuhimu wa Afya na Usalama katika maeneo ya kazi ikiwa ni katika kutekeleza mpango mkakati wa Dunia wa kumaliza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Mkutano huu umebeba kauli mbiu inayosema “UKIMWI bado ni Ajenda Endelevu” yaani “AIDS is an unfinished Business.” Mkutano huu, Utatafuatiwa na mafunzo ya siku tatu wa Wakufunzi wa Rika “Peer Educators Training” yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusiana na masala ya UKIMWI na Afya katika maeneo ya kazi. Mafunzo haya yamebeba kaulimbiu inayosema “Mafunzo kwa Waelimishaji Rika katika Maeneo ya Kazi ni Msingi Endelevu katika mapambano dhidi ya UKIMWI: Wakati ni sasa” yaani Workplace Peer Education is Key for Sustainability of HIV/Wellness Programs: Time to Act!”
Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suazanne Ndomba-Doran akitoa salamu za ukaribisho, ameeleza mchango mkubwa unaotolewa na ATE katika kuzikutanisha Sekta Binafsi na Wadau kupitia Programu mbalimbali za afya na masuala ya UKIMWI katika maeneo ya Kazi kwa kuzingatia Dunia iko katika mpango mkakati wa kumaliza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Bi. Ndomba-Doran ameongeza kuwa pamoja na hatua kubwa ambazo Tanzania imepiga katika kutokomeza UKIMWI, bado kuna kazi kubwa ya kufanya na wadau wote ili kupata Tanzania isiyo na VVU/UKIMWI na kuwa ATE kwa kushirikiana na Serikali na Wadau wengine wataendelea kuunga mkono juhudi zote za kufikia lengo ifikapo mwaka 2030.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini ( TUCTA), Bw. Herry Mkunda ambaye pamoja na mambo mengine amewaomba wadau wote kuendeleza ushirikiano katika kuhamasisha masuala ya UKIMWI na Afya na Usalama mahala pa Kazi ili kufikia malengo ya mkakati wa 95% hadi kufikia mwaka 2030.
Mkutano huu umehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkaazi wa UNAIDs, Dkt. Martin. Ordiit, Mwakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ( TACAIDs), Mwakilishi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi pamoja na wadau mbalimbali wa Masuala ya UKIMWI kutoka ndani na nje ya Nchi.
Post Comment
No comments