UVCCM YATOA UFAFANUZI JUU YA MKATABA WA BANDARI KATI YA DP WORLD NA TANZANIA
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) taifa umesema nia ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dokta Samia Hassan ni njema juu ya uwekezaji wa bandari Tanzania na kuwataka wananchi kuunga mkono na kuwapuuza wapotoshaji juu ya azimio la Bunge la mapendekezo ya kuridhia makubaliano juu ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji Kazi wa Bandari Tanzania la Mwaka 2023.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Kawaida amesema kinachofanyika sio kitu alichoamua mtu binafsi bali ni maelekezo ya chama kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 hadi 2025.
Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia mkataba wa Mashirikiano na Serikali ya Dubai kwa kuanzisha ushirikiano wa kuboresha, kuendesha na kuendeleza maeneo ya Bandari nchini ili ufanisi wake uwe wa viwango vya kimataifa.
Kawaida amebainisha kuwa mkataba huo umekusudia kuleta tija na ufanisi wa Bandari suala ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa Serikali katika kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii.
Pia aliongeza kuwa majadiliano na Maandalizi ya mkataba huo yamefanywa na timu ya wataalam wa Tanzania ambao wana uzoefu mkubwa katika masuala ya mikataba ya kimataifa na kabla ya kusainiwa ikizingatia taratibu zote za Nchi.
"Ushirikiano ulioanzishwa pamoja na mambo mengine unajikita kwenye kuboresha uendeshaji wa shughuli za Bandari nchini kwa kuongeza tija na ufanisi, kusimika mifumo ya kisasa ya TEHAMA na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo Watanzania katika uendeshaji wa shughuli za Bandari" Alisema Bw. Kawaida
Pia Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kueleza utaratibu wa makubaliano ambayo Serikali ya Tanzania inaingia na Serikali ya Dubai lengo likiwa ni kupunguza upotoshaji.
Alisema utaratibu huo wa makubaliano unahusisha hatua kubwa tatu ambazo ni makubaliano baina ya Serikali na Serikali (Intergovernmental Agreement), makataba wa Nchi mwenyeji (Host Government Agreement) na mikataba mahususi ya utekelezaji wa huduma (Definitive Agreement - Concession or Service Level Agreement).
No comments