Breaking News

MABENKI NCHINI YAPENDEKEZA KUUNDWA KIKOSI KAZI KUANDAA MIONGOZO UKOPESHAJI WACHIMBAJI WADOGO


Asteria Muhozya na Bibiana Ndumbaro- Dar
Taasisi za Fedha nchini zimeshauri kuundwa Kikosi Kazi kitakachohusisha taasisi hizo na nyingine ikiwemo Wizara ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Vyuo Vikuu na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) ili kuandaa miongozo ya ukopeshaji kwa wachimbaji wadogo.

Ushauri huo umetolewa baada ya kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wachimbaji wadogo ambayo kwa kipindi kirefu imekua kikwazo katika kutekeleza shughuli zao na hivyo kuibua mijadala ya mara kwa mara katika Sekta ya Madini.

Kwa kuitambua changamoto hiyo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limewakutanisha Wachimbaji Wadogo wa Madini na Wadau wa Madini ya Viwandani zikiwemo taasisi za fedha ili kujadili namna ya kutatua changamoto hiyo.

Aidha, pamoja na kutolewa kwa pendekezo hilo, akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mabenki Nchini (TBA) AbdulSaid Msombe amesema  wachimbaji wadogo nchini wanapaswa kuzingatia masuala kadhaa ya msingi ambayo yatawawezesha kukopa katika mabenki na kuyataja baadhi kuwa ni pamoja utunzaji wa  kumbukumbu za manunuzi na matumizi, kuwa na akaunti katika benki ili kuzirahisishia benki kutoa mikopo.

Msombe ameyataja  mengine kuwa ni pamoja  na kuhakikisha wanakua na mfumo mzuri wa uendeshaji, kufuata  taratibu za kiserikali ikiwemo usajili ili  kufahamika kisheria pamoja na  kuwa na  taarifa zinazoonesha mikataba wanayoingia ikiwemo ya mahali wanaponunua madini, mahali wanapopata  huduma, kuzingatia masuala ya kuingia mikataba na watoa huduma mbalimbali.

Msombe ameyasema hayo wakati  chama hicho na wawakilishi kutoka benki mbalimbali nchini zikiwemo CRDB, NMB, Azania benki na NBC walipotoa mada kuhusu namna benki hizo zinavyoweza kufanya kazi katika sekta ya Madini hususan kushirikiana na wachimbaji wadogo katika Mkutano wa Wachimbaji Wadogo wa Madini na Wadau wa Madini ya Viwandani uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Chama Cha Wachimbaji Madini Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI)  

Katika hatua nyingine, Msombe amesema kutokana na Sekta ya Madini kuwa ngeni katika shughuli za kibenki, amesema nguvu kubwa inayowekwa na taasisi hizo hivi sasa ni kutoa mikopo katika hatua ya uzalishaji wa madini hayo ikiwemo mikopo ya vifaa.

Aidha, taasisi hizo zimeiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa mabenki nchini kuhusu shughuli za sekta ya madini ili kuziwezesha kupata ufahamu na uelewa wa kutosha kuhusu biashara ya madini kuziwezesha kutoa mikopo kwa wachimbaji ili pande zote ziweze kunufaika kikamilifu.

Pamoja na kutoa mawasilisho, taasisi hizo zimepata fursa ya kuelezea kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hizo ambazo zitawawezesha wachimbaji kupata mikopo.  

Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kuleta matokeo chanya yatakayoleta suluhisho la pamoja ili kuleta mapinduzi katika sekta hii ya uchimbaji mdogo wa madini ya viwandani.



No comments