WATU WAKIRUDI KWENYE MFUMO WA 'CASH MONEY' SERIKALI ITAPOTEZA FEDHA NYINGI- WAKILI OLENGURUMWA
Wakili Onesmo Olengurumwa ambaye ni Mratibu wa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini (THRDC) ametoa maoni binafsi kuhusu tozo
mpya kwenye miamala ya huduma za kibenki ambapo amesema kuwa zitapelekea
wananchi kurudi kwenye utamaduni wa zamani wa kutunza pesa kwenye vibubu na
kutembea na pesa taslimu (cash money) hali ambayo amedai kuwa inaweza kuleta
madhara kiuchumi.
Akizungumza baada ya kuibuka kwa mijadala kuhusu tozo mpya
kwenye miamala ya huduma za kibenki ambazo zimeanza kutozwa hivi karibuni baada
ya mwaka mpya wa fedha 2022/2023 kuanza, amesema kuwa watanzania bado
watanzania walio wengi hawatumii huduma za kibenki hivyo kuwekwa kwa tozo hizo
kutafanya watanzania kurudi kwenye mifumo ya kizamani ikiwemo kutunza pesa
kwenye vibubu pamoja kukaa na pesa taslimu (cash money) hali ambayo amedai kuwa
inapelekea madhara kwenye uchumi.
"Watanzania wanaotumia benki hawafiki hata asilimia
tano(5%) sasa ukienda kuingiza ghalama za kuweka na kutoa pesa kwenye benki
unafanya watanzania warudi kwenye mifumo ya vibubu kuweka pesa majumbani,
warudi kwenye cash money (pesa tasrimu), Cash money ina madhara sana kwenye
uchumi."amesema Wakili Onesmo Olengurumwa
Wakili Olengurumwa ameongeza kuwa "Watu wakirudi kwenye
mfumo wa cash money Serikali itapoteza pesa nyingi sana lakini Serikali
itashindwa hata kupambana na uharifu wa kifedha kwa sababu kupia mifumo hii ya
simu, mifumo ya benki ni rahisi kufahamu mtiririko wa pesa inatoka wapi inaenda
wapi."
Aidha ameshauri ili kuepuka hali ya sintofahamu inayoleta
mijadala na malalamiko awali inapokuwa inafanyika michakato yoyote kwenye
kuboresha uchumi hususani kuongeza vyanzo vya mapato katika taifa vinavyogusa
wananchi kuwa ni muhimu kuwepo na mijadala ya awali pamoja na ushirikishwaji wa
kutosha kwa jamii.
"Tunapojaribu kufanya michakato yoyote ya kuboresha uchumi wetu, kuboresha vipato vya kitaifa lazima tuangalie na tunapogusa mambo ya kitaifa yanayogusa watanzania kama suala la tozo kwenye miamala tunapasa kuanza na mijadala ya kitaifa ndio maana nasema vitu vingi vinakuja pasipo ushirikishwaji mkubwa wa jamii. Sidhani kama watanzania wameshawishiwa na mh. Rais pamoja na wa wadau wengine kwamba wachangie halambee ya kuchangia maendeleo ya taifa lao kwa njia nyingine kama kupitia tozo na vingine, ikiwa hivyo hamna tatizo" amesema Wakili Onesmo Olengurumwa
Katika hilo amesema kuwa wananchi wamekuwa wakiona baadhi ya
mambo yakiibuka ikwemo kufanya marekebisho ya sheria na vifungu ambavyo
vinakuja kuwabana.
"Kitu kinachoonekana hapa mambo yameibuka na kuzuka
wananchi wanayaona yakiwajia sheria zinafanyiwa marekebisho, vifungu vinawekwa
vinakuja kuwabana watanzania na hali tuliyonayo yakiuchumi vijana wanaangaika
kutafuta rasilimali ukiwaongezea mazingira kama hayo hali inakukwa ngumu"
amesema Onesmo Olengurumwa
Hata hivyo Wakili Onesmo Olengurumwa ameshauri wadau kutoishia tu kwenye mijadala na kutoa malalamiko badala yake watumie Mahakama ili iweze kutoa tafsiri uhalali wa tozo hizo.
No comments