PROF. NDALICHAKO: SERIKALI KUFANYA KUBORESHO YA SERA YA TAIFA YA VIJANA, KUUNDWA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Profesa Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa ufunguzi wa Tuzo za Vijana Wanaochipukia za mwaka 2022 zilizoandaliwa na taasisi ya Africa Youth Transformation katika ukumbi wa maktaba mpya jijini Dar es salaam.
Meneja kampeni na utetezi wa taasisi ya Save the Children Bi. Jovitha Mlay akifafanua juu ushiriki wa taasisi hiyo katika Tuzo za Vijana Wanaochipukia za mwaka 2022 zilizoandaliwa na taasisi ya Africa Youth Transformation katika ukumbi wa maktaba mpya jijini Dar es salaam.
Dar es Salaam:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za maboresho ya Sera ya Taifa ya Vijana ambayo itahusisha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Tuzo za Vijana Wanaochipukia za mwaka 2022 zilizoandaliwa na taasisi ya Africa Youth Transformation, Profesa Ndalichako amesema serikali ipo katika mchakato wa kuipitia Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 kisha itawaalika vijana hili kutoa maoni na mapendekezo yao.
"Sera hii itakapokamilika, itaenda sambamba na Baraza la Vijana ambalo litatoa fursa kwa vijana kutoa maoni yao na kuishauri Serikali ili sera hiyo ibebe mahitaji ya vijana wa sasa." Alisema Profesa Ndalichako.
Alisema sera hiyo siyo tu itawaunganisha vijana, bali itaondoa tofauti za kisiasa kwa maslahi ya taifa na kuwaweka vijana pamoja licha ya tofauti zao.
Akizungumzia mikopo ya vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana Profesa Ndalichako alisema Serikali imepunguza masharti ya kutoa mikopo kwa vijana ikiwemo kuongeza muda wa kurejesha mkopo kutoka miezi 24 hadi miezi 36 na kuongeza kiwango cha mkopo kutoka Sh10 milioni hadi Sh50 milioni.
"Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa vijana hili kwa lengo la kuchochea ajira, Uvumbuzi na ubunifu wanaofanya vijana katika kujikwamua kimaisha"
Naye Meneja kampeni na utetezi wa taasisi ya Save the Children Bi Jovitha Mlay amesema lengo la kushiriki katika uandaaji wa tuzo hizi ni kutambua mchango wa vijana Katika kukuza uchumi.
Amesema taasisi yao imeshiriki kupitia makundi mbalimbali ya vijana ikiwemo, Mabadiliko ya tabia ya nchi na "Green business', Ulinzi wa watoto, Afya ya uzazi pamoja na teknolojia
Bi. Mlay ameongeza kuwa Save The Children inaamini kama vijana watajengewa mazingira wezeshi, kisera, kimkakati, kirasilimali, mafunzo pamoja na taarifa wanaweza kufanya mambo ambayo yatakuza uchumi wa nchi.
Tuzo za Vijana TEYA 2022 zinatolewa kwa lengo la kuwezesha vijana kuonyesha mchango wao na vipaji walivyonavyo mwaka huu zimebeba kaulimbiu ya "Jionyeshe Tukuonyeshe: Tengeneza Fursa kwa Vijana."
No comments