Breaking News

STAMICO, KCB WASAINI MAKUBALIANO KUWAPATIA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI MIKOPO ISIYO NA RIBA

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Vennance Mwasse (wa pili kulia) na Mwakilishi wa Benki ya KCB, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kiislamu (Islamic Banking) BW. Amour Muro (wa pili kushoto) wakikabiadhiana hati za makubaliano mara baada ya kumalizika zoezi la utiaji saini.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Vennance Mwasse (kulia) na Mwakilishi wa Benki ya KCB, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kiislamu (Islamic Banking), Bw. Amour Muro wakisaini hati za makubaliano na mashirikano kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Vennance Mwasse akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari (hawamo pichani) mara baada ya utiaji saini wa Makubaliano hayo, (kushoto) ni Mwakilishi wa Benki ya KCB, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kiislamu (Islamic Banking), Bw. Amour Muro. 
Mwakilishi wa Benki ya KCB, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kiislamu (Islamic Banking), Bw. Amour Muro akielezea namna mikopo hiyo kwenye hafla hiyo.

Na: Mwandishi wetu
Wachimbaji wadogo wa madini nchini wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia habari njema ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Benki ya KCB kuingia makubaliano yanayolenga kushirikiana katika kutoa mikopo ya kuwawezesha kupata mikopo endelevu na kwa rahisi zaidi ili  waweze kufanya shughuli za uchimbaji zenye tija.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya STAMICO kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wake, Dkt. Vennance Mwasse amesema mikopo hiyo inategemewa kuleta tija kwa wajasiliamali lakini pia kwa taifa.

“Mpaka sasa wachimbaji wadogo wanaongoza kwa kupatiwa leseni ukizingatia na wadau wengine, kimsingi unaposema  wachimbaji wadogo maana yake ni wazawa, hadi sasa leseni 34,000 zimeshatolewa, makubaliano haya yatawasaidia watanzania kuleta tija katika biashara zao,” alisema Dkt Mwasse

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kusaini Hati ya makubaliano (MOU) baina ya pande hizo mbili Novemba 16, 2021 katika Ofisi za STAMICO Jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa Makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Vennance Mwasse amesema kuwa Malengo ya makubaliano hayo ni kushirikiana na Taasisi za fedha katika kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mikopo endelevu na yenye tija.

"Katika Makubaliano haya STAMICO itawajibika kutoa utaalam elekezi katika maeneo ya Jiolojia, Uchimbaji na Uchenjuaji Madini kwa miradi ya Wachimbaji Wadogo ambayo itafanya maombi ya mikopo na kuiwasilisha kwa Benki kabla ya utekelezaji wake na Benki ya KCB itawajibika kutoa mikopo kwa Wachimbaji Wadogo ambao watawasilisha maombi ya mikopo katika maeneo ya miradi ya uchimbaji madini itakayokidhi vigezo vya kupewa mikopo.Amesema Dkt. Mwasse.

Ameongeza kuwa Makubaliano hayo yatadumu kwa muda wa miaka mitatu (3) kuanzia mwaka huu wa 2021 ambapo pia yanaweza kufanyiwa mapitio kila baada ya mwaka mmoja.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya KCB, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kiislamu (Islamic Banking), Bw Amour Muro amesema wafanyabiashara ambao wanaogopa kukopa kwa sababu ya riba sasa hawana cha kuogopa kwa sababu wako tayari kutoa mikopo hiyo bila riba yeyote.

Aidha amesema suala la riba halibagui dini, mfanyabiashara yeyote anayetaka kukopa bila kula ripa anachopaswa ni kusema na KCB wako tayari kuwahudumia.

Aidha Mtaalamu huyo wa mambo ya fedha amesema ametoa wito kwa wachimbaji wadogo waislam na wasio waislam kujitokeza kuchukua mikopo isiyo na riba.

"Mpaka sasa Benki yetu tayari imeshatoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4 kwa wateja wetu wote na sasa tupo tayari kuwafikia wachimbaji wadogo kwa kuwakopesa ili waweze kufanya shughuli zao" Amesema Amour.

STAMICO imendelea kutekeleza mikakati yake ya kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo nchini ili uwe wenye tija na kuchangia ipasavyo uchumi wa nchi ikiwa ndio Mlezi wa Wachimbaji Wadogo hapa nchini.

Mwanasheria wa Benki ya KCB Antonia Kilama (kushoto) akikamilisha zoezi la utiaji saini makubaliano, (kulia) Mwanasheria wa STAMICO Robert Ambrozi akishuhudia tukio hilo katika hafla iliyofanyika Ofisi za STAMICO Jijini dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Vennance Mwasse (kulia) na Mwakilishi wa Benki ya KCB, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kiislamu (Islamic Banking), Bw. Amour Muro (kushoto) wakibadilishana hati za makubaliano mara baada ya kutia saini makubaliano ya mashirikano katika kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo Jijini Dar es Salaam. Picha zote kwa hisani ya HUGHES DUGILO.

No comments