Breaking News

SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI NA WEZESHI KWA SEKTA YA UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imezindua rasmi miradi mikubwa 6 kwa Tasnia hiyo ikiwemo:-

1. Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa;
2. Uzinduzi wa Mfumo wa Kidigitali wa BASATA;
3. Uzinduzi wa Mfumo wa Kidigitali wa Bodi ya Filamu;
4. Uzinduzi wa Mfumo wa Kidigitali wa COSOTA;
5. Uzinduzi wa Samia Taifa CUP; na
6. Uzinduzi wa mkakati wa kujenga umoja na Wadau wa Tasnia.

Katika Hafla hiyo, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa alieleza kuwa, lengo la Serikali ni kurahisisha utendaji wa Wadau wa Sanaa na ndio maana imekuja na mikakati hiyo 6 ikiwa ni sehemu ya kuenzi mafaniko ya miaka 60 ya Uhuru kwa Sekta hiyo.

"kuanzisha Bodi ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, sio tu kuitikia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, bali ni kuitikia kilio cha Wadau cha kuwa na mfuko utakaosukuma mawazo, miradi, na ubunifu wao" alisema Mhe. Bashungwa.

Aidha, Mfuko huo tayari umetengewa Shilingi bilioni 1.5 ambapo utasaidia Wanatasnia kupata mikopo ya masharti nafuu, pamoja na mafunzo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alieleza faida zitakazopatikana kwa Wadau wa Filamu nchini kupitia mfumo wa Kidigitali uliozinduliwa. 

Alisema kuwa, mfumo utaondoa usumbufu kwa Mdau wa Filamu wa kulazimika kuja ofisini kufuata huduma, ambapo sasa ataweza kupata huduma popote atakapokuwepo ikiwemo, Vibali vya kutayarisha Filamu, Vibali vya Uhakiki na Vitambulisho. 

Aidha, mfumo utarahisisha utoaji wa huduma, ambapo Mtayarishaji wa ndani atapata kibali ndani ya siku 1 badala ya siku 30, kwa Waombaji wa nje watapata vibali ndani ya siku 3 badala ya siku 30, halikadhalika Vibali vya Uhakiki ndani ya siku Tatu.

Alimalizia kwa kusema kuwa, mfumo utatunza kumbukumbu itakayosaidia kupanga Mipango ya maendeleo kwa Wadau wa Filamu ikiwemo utoaji wa mafunzo.
Naye Raisi wa Shirikisho la Filamu Bw. Eliya Mjatta alitoa rai kwa Wadau wa Filamu nchini kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za Serikali kwa kutumia mifumo hiyo ya Kidigitali ili kurahisha utendaji wa kazi zao.


No comments