Breaking News

Waziri Mkuu MAJALIWA Mgeni Rasmi Ufunguzi Maonyesho Ya Nne Ya Madini GEITA 2021

NA Tunu Bashemela.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye  ufunguzi wa maonyesho ya Teknolojia na uwekezaji katika Sekta ya Madini yatakayofanyika mkoani Geita kuanzia Septemba 16 hadi 26 mwaka huu.

Hayo yalibainishwa leo jijini Dar es Salaam  na Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemarry Senyamule, katika Ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) alipokuwa na Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo.

"Maandalizi ya maonyesho haya yanakwenda vizuri mpaka sasa. Maonyesho haya ni fahari ya Mkoa wa Geita," alisema Senyamule.

Senyamule alieleza kuwa  Mkoa wa Geita ndio mkoa ulioanzisha maonyesho ya madini nchini na kuhamasisha wadau kushiriki kila mwaka.

Aliongeza kwa kusema kwamba kwa mwaka huu ni maonyesho ya nne hivyo aliwataka wadau na wananchi ambao hawakushiriki mwaka jana wasipange kukosa mwaka huu.
Senyamule alisema kuwa maonyesho hayo yatakuwa ya kimataifa kwasababu yatashirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

"Imezoeleka maonyesho haya kufanyika kitaifa na kuhudhuliwa na wadau na wawekezaji wengi wa ndani kwa takriban miaka mitatu na mwaka huu wanne utakuwa wa kipekee sana," Alisema Senyamule.

Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa maonyesho hayo yatajumuisha mnyororo wa wadau katika Sekta ya Madini yaani kuanzia mchimbaji hadi anayetengeneza madini kwa hatua ya mwisho.

Alitoa wito kwa wajasiriamali wadogo wa Mkoa wa Geita kuchangamkia fursa za kuichumi katika kipindi hicho cha maonyesho hayo ili kuweza kunufaika kibiashara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Geita James Chiragi alieleza jinsi walivyojipanga katika maonyesho hayo, na mategemeo ya kupokea wageni wengi katika maonyesho hayo.

Chiragi pia alisema kuwa kutakuwa na kitu kipya kitakachofanyika kwenye maonyesho hayo, ambayo ni kuwepo kwa kiwanda cha kusafishia madini kwa Mkoa wa Geita ili kutosambaza na kusafirisha tena dhahabu ghafi pamoja na kusambaa dhahabu zilizokwisha safishwa kikamilifu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maonyesho ya dhahabu Geita, Eng Chacha Wambura akizungumza kwa niaba ya wafanya bishara binafsi, aliwakaribisha wafanyabishara wote kuja kuchangamkia fursa kwenye maonyesho hayo,akisema yeye ni shuhuda wa maonyesho yaliyopita kwa wajasiliamali na wafanya biashara walivyonufaika kwa kupata faida kupitia maonyesho hayo.

 

No comments