Wakala wa Vipimo Yawadaka Wafanyabishara Wawili Kwa Udanganyifu Jijini Dar
Kaimu Meneja wa wakala wa vipimo (WMA) mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam Charles Mavunde akiongea na vyombo vya habari baada ya kuwakata wafanyabiashara wawili wasio waaminifu ambao walikuwa wakiuza mafuta ya kula kwa kupunja kipimo chenye ujazo wa lita 10 na 20 kwa kuweka ujazo wa mililita 750 hadi lita moja (Picha na Bakari Lulela)
Na Bakari Lulela
IMEELEZWA kuwa ukaguzi wa bidhaa zinazofungashwa na vipimo unaoendelea kufanywa na Wakala wa vipimo (WMA) mkoa wa kinondoni jijini Dar es Salaam umefanikiwa kuwakamata wafanyabiashara wawili (majina yamehifadhiwa) wanaouza mafuta ya kula waliobainika kupunja ujazo wa mafuta madumu ya lita 10 kwa kupunja ujazo kwa wastani wa mililita 750 hadi lita moja.
Amesema wafanyabiashara hao wasio waaminifu walikamatwa katika maeneo tofauti ambapo mmoja kwenye kata ya Magomeni na mwingine katika kata ya Mwananyamala na kufikishwa kwenye ofisi ya wakala wa vipimo kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya vipimo sura 340, wafanyabiashara hao wawili walitozwa faini pamoja na kupewa onyo la kutorudia kosa hilo.
Akitoa taarifa hizo kupitia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Kaimu Meneja wa Wakala wa vipimo (WMA) mkoa wa Kinondoni Mh. Charles Mavunde alisema kama Wakala wa vipimo wamebaini wafanyabiashara wasio waaminifu wakiuza bidhaa za mafuta ya kula yakiwa katika hali ya kupunjwa kipimo katika vifungashio vya lita 10 na lita 20.
"Katika ukaguzi tunaoufanya tumebaini uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiuza bidhaa za mafuta ya kula yakiwa yamepunjwa kipimo ndani ya vifungashio vya madumu yenye lita 10 na 20," alisema Mavunde
Mavunde alisema kuwa wao kama wakala wa vipimo wataendelea kuhakikisha bidhaa mbalimbali zinazofungashwa viwandani ikiwemo sukari,mafuta ya kula, Sementi n.k toka kuzalishwa kwake na kufungashwa viwandani zinapoingia sokoni zinatakiwa ziwe na ujazo au uzito sahihi kulingana na kiasi kinachokuwa kimeandikwa katika kifungashio.
Aidha Kaimu Meneja huyo alisema ni makosa kwa mujibu wa sheria ya vipimo kwa mfanyabiashara mzalishaji kuuza bidhaa ambazo vipimo vyake vilivyoandikwa kwenye kifungashio kikiwa tofauti na kiasi halisi kilichomo katika kifungashio, hata hivyo Wakala wa vipimo wanawahakikishia wananchi kwamba, watahudumiwa kwa kutumia vipimo vilivyohakikiwa kwa usahihi bila kupunjwa bidhaa kwa kuwa ndo jukumu la taasisi hiyo.
"Kwa mujibu wa sheria ya vipimo sura 340 ya mapitio mbalimbali shughuli zetu za Wakala wa vipimo ni kumlinda mlaji kupitia uhakiki wa vipimo vinavyotumika katika biashara pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa," alisema Kaimu Meneja huyo.
Wito umetolewa kwa wananchi waweze kutoa taarifa mara wanapobaini wafanyabiashara wasio waaminifu katika upunjaji wa bidhaa wakiuza zikiwa zimefungashwa huku wengine wakitumia vipimo visivyo hakikiwa na Wakala wa vipimo.
WMA imewasisitiza wananchi kwamba utaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo ya biashara, kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo na ufungashaji bora wa bidhaa zinazozalishwa viwandani ili kuongeza tija.
Post Comment
No comments