Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma Bi.Gaudencia Simwanza akizungumza katika kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro kilichofanyika mkoani Morogoro kilichoandaliwa na TMDA. Waandishi wa habari wakifuatilia kwa ukaribu Mada zinazowasilishwa katika kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro kilichofanyika mkoani Morogoro kilichoandaliwa na TMDA.

NA EMMANUEL MBATILO

Baadhi ya majukumu ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuhakikisha afya ya mwananvhi inalindwa ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopo katika soko ni salama na zenye ubora.

Ameyasema hayo Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro       Bw.Anza Ndossa ambaye aliweza kuhudhuria katika kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro uliofanyika mkoani Morogoro.

Akizungumza katika kikao hicho Bw.Ndossa amesema TMDA inajukumu la kusimamia matangazo ya bidhaa za dawa na vifaa Tiba ili kuzuia matangazo yenye nia ya kupotosha Umma kwa lengo la biashara ambapo matangazo ya namna hiyo hutolewa na vyombo vya habari na mitandaoni.

“Suala la kudhibiti matangazo ni la kisheria na katika kuhakikisha utekelezaji wake zipo kanuni za udhibiti wa matangazo ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi zilizoandaliwa chini ya sheria ya dawa na vifaa tiba sura ya 219 zilizoanza kutumika mwaka 2010 ambapo ni takribani miaka 10 imepita”. Amesema Bw.Ndossa.

Aidha amesema kuwa kati ya changamoto kubwa ambazo Mamlaka imekumbana nazo kutoka kuanzishwa kwake ni kushuhudia matangazo ya bidhaa zinazodhibiti kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii bila kujali kibali cha TMDA kinyume na matakwa ya kisheria na kanuni hiyo kuchangia kupotosha jamii.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),Bw. Akida Khea akiwasilisha Mada isemayo “Mchango wa TMDA katika Kutekeleza Sera ya Viwanda” amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Tanzania pamoja na mambo mengine imeweka msukumo mkubwa katika uanzishwaji wa viwanda hapa nchini ikiwemo viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu, mifugo na vifaa tiba.

Aidha Bw.Khea amesema Wawekezaji 16 wapya waliwasilisha maombi ya usajili wa viwanda vipya vya dawa na vifaa tiba ambavyo kwa sasa vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Pamoja na hayo Bw.Khea amesema Viwanda vipya vimelenga kuzalisha dawa zifuatazo

–Dawa za sindano (Sterile Small Volume Parenteral (SVP) and Large Volume Parenteral (LVP))

–Chanjo (veterinary vaccines)

–Dawa za macho (Sterile ophthalmic)

–Dawa za kupaka (Topical preparations)

–Dawa za vidonge na maji (General Oral Solid Dosage forms & oral liquids).

“Kwa sasa kuna jumla ya viwanda 14 vya ndani vilivyosajiliwa; 7 – dawa za binadamu, 2 – dawa za mifugo  na  5 – vifaa tiba hii ni hatua kubwa ambayo wamefikia”. Amesema Bw.Khea

Katika maazimio ya kikao kazi hicho ni pamoja na TMDA kuendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari,kutumia viongozi mbalimbali wa dini na wa kimila,kutoa elimu kwa makundi maalum, kutoa waraka kwa vyombo vya habari juu ya udhibiti wa matangazo,TMDA kukutana na uongozi wa TCRA kuhusu udhibiti wa matangazo,vikao vya mara kwa mara na waandishi habari pamoja na kuandaa ziara ya waandishi kutembelea maabara ya mwanza.