Breaking News

Makumbusho ya Taifa Waibuka na Mkakati wa KIDIJITALI



Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akifafanua jambo kwenye kikao kazi cha Mkakati wa kuanzisha mfumo wa Uduma za Kimakumbusho kidijitali.
Pichani Mtaalam wa Software Engineering Bw Edward Pius akielezea namna mfumo wa Uduma za Kimakumbusho kidijitali utakavyo fanya kazi na faida zake.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga na wajumbe wengine wakijadiliana juu ya mfumo wa Uduma za Kimakumbusho kidijitali 

Na Sixmund J, Begashee
Shirika la Makumbusho nchini limeanza mkakati wa kuwawezesha watalii kote duniani kuitembelea Makumbusho za Taifa nchini kwa njia ya kidigitali ili kutoa wigo na fursa pana kwa wadau na wapenzi mbali mbali wa Makumbusho kupata nafasi ya kujionea Maonesho, kujifunza na hata kuburudika kwa kupitia TEHAMA.

Akizungumza katika kikao kazi maalum kilicho wakutanisha wataalam wa TEHAMA na habari wa Makumbusho hiyo  pamoja na wataalam wa Software Engineering (kutoka nje ya Makumbusho ya Taifa) Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Lwoga alisema  lengo la kikao kazi hicho ni kujadiliana na kubadilisha uzoefu wa njia bora na yaharaka ya kuipeleka Taasisi hiyo kwenye mfumu wa kidijitali.

“Nimeona ni vyema tuondoke hapa tulipo na tuwafuate wadau na watu mbali mbali wanaopenda kuzitembelea Makumbusho zetu kidijitali maana naamini hii ndio njia rafiki kwa watu wengi hasa walio mbali na huduma zetu hususani vijana na kwa kuwa teknolojia inakwenda kasi vivyo hivyo na sisi Makumbusho tunatakiwa twende na kasi hiyo. Alisema Dkt Lwoga

Akielezea namna mfumo wa “e- MAKUMBUSHO” utakavyo fanya kazi na faida zake, mmoja wa wataalam wa Software Engineering alisema, mfumo huo utawawezesha hata watu wenye Ulemavu, watu wa mataifa mbali mbali Duniani wasio na uwezo wakusafiri kufikiwa na huduma za Kimakumbusho lakini pia itasaidia kuongeza mapato kwa kuwa watu wataweza kuitembelea Makumbusho masaa yote kupitia simu zao za mkononi na kompyuta wakiwa popote pale. 

Akimpongeza Mkurugenzi Mkuu kwa utendaji wake wa kazi kwa kasi, Mkurugenzi wa Kituo cha  Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam Bw Achiles Bufure amesema kuwa Mkakati huu umekuja wakati muafaka hasa katika changamoto hii ya janga la kidunia la Virusi vya Korona (COVID 19) vinavyo sababisha homa kali ya Mapafu ambalo limewafanya watu wengi kusitisha kutembelea sehemu za kitalii kikiwemo kituo cha Makumbusho hiyo.

“Tumekuwa tukipata wageni wengi hasa wanafunzi wakiitembelea Makumbusho yetu kwa lengo la kujifunza kupitia kumbi za maonesho, kuburudika kupitia Ukumbi wetu wa kisasa wa Maonesho ya Jukwaani, Maktaba ya wazi kwa wote na ile ya watoto, wateja wa kumbi za mikutano na viwanja vya wazi lakini sasa idadi ya wateja wetu hao imepungua sana, sasa kwa hii “e-MAKUMBUSHO” tutakuwa tumezifikisha huduma zetu viganjani mwa wengi.’’ Aliongezea Bw Bufure.

Katika utekelezaji wa mkakati huu, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Lwoga amesema ataunda timu ya wataalam kutoka Taasisi mbali mbali za serikali wakishirikiana na wataalam wa ndani ili kuhakikisha lengo lililopo linakamilika kwa wakati mfupi lakini pia kwa ubora unaotakiwa.

No comments