Bara La AFRIKA Kugawanyika Mara Mbili
Wanajiolojia
wameeleza kwamba Tanzania na baadhi ya nchi nyingine za Afrika, zitameguka na
kuwa visiwa.
Hata hivyo,
wamesema mchakato huo utachukua mamilioni ya miaka.
Wamesema kuibuka
kwa ufa mkubwa katika eneo la Bonde la Ufa, Kusini Magharibi mwa Afrika
kutasababisha nchi za Kenya, Tanzania, Djbouti na Msumbiji kumeguka.
Pamoja na hayo,
mjiolojia mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Ndogoni
alisema kuwa kumeguka huko kutasababisha baadhi ya nchi za Afrika ambako
Bonde la Ufa linapita kuzungukwa na bahari.
“Zitakuwa kama
ilivyo kwa visiwa vya Madagascar au Zanzibar,” alisema.
Ndogoni alisema
kwa waliosoma Jiografia, mchakato huo ni kama ule wa kugawanywa kwa mabara
saba, “Zile nguvu za kupasuka kwa miamba hadi yakawepo mabara saba duniani bado
zinaendelea. Mkondo huu wa Bonde la Ufa, ulianzia Kaskazini mwa Afrika katika
nchi za Djibouti, Kenya mpaka Kusini mwa Tanzania.”
Alisema mkondo wa
kwanza upo Ethiopia na kwa upande wa Kenya kuna miwili ambayo mmoja ndio
uliopita hadi katika baadhi ya maeneo ya Tanzania kama Manyara, Singida, Iringa
na Mbeya.
Alisema kasi ya
maeneo hayo kujitenga ni milimita 0.1 Kusini mwa Afrika na milimita 6.5
Kaskazini mwa Afrika na kwamba Tanzania ipo katikati ya maeneo hayo.
“Kumeguka huku kwa
bara la Afrika kunaleta wasiwasi kwa sababu kunatokea katika makazi ya watu,”
alisema.
Dk James Hammond
wa Idara ya Sayansi na Uhandisi kutoka Chuo cha Imperial cha London alinukuliwa
na jarida la mtandaoni la Mail & Guardian akisema, “Katika miaka milioni
kadhaa ijayo, shughuli hii itakamilika na kuigawa Afrika mara mbili, na kuunda
bahari mpya hapo katikati. Ukitumia jiografia ya sasa, bara hilo jipya
litashirikisha Somalia, nusu ya Ethiopia, Kenya na Tanzania.”
Baadhi ya
wanajiolojia wanakadiria kwamba huenda mpasuko huu ukayabeba pia mataifa ya
Uganda, Rwanda, Burundi na maeneo ya Malawi na Msumbiji.
Hivi karibuni,
maofisa wa Mamlaka ya Taifa ya Barabara Kenya (KeNHA) wakishirikiana na
mkandarasi kutoka China anayejenga reli ya kisasa, walifika katika bonde hilo
kuziba baadhi ya nyufa.
Baada ya
uchunguzi, ilibainika kwamba hali hiyo ilitokana na shughuli ya kijiolojia
chini ya ardhi ambayo ilihusisha mvutano wa vipande vikubwa vya ardhi.
Siku chache
baadaye, ufa huo uliendelea kupanuka na kuathiri barabara hiyo tena jambo
lililosababisha magari yenye kubeba mizigo mizito kushindwa kupita. Pia ufa huo
ulianza kuathiri nyumba za wakazi.
“Mkandarasi na wahandisi wako hapo kwa sasa na
watabaki ili kufuatilia yanayojiri kutokana na shughuli za kivolkano ambazo
zilisababisha ufa huo,” naibu mkurugenzi wa mawasiliano wa Kenya, Charles Njogu
alisema baada ya ukarabati huo mara ya kwanza.
No comments