Kutoka Shinyanga: Mwenyekiti Wa Kijiji Asimamishwa Kazi Kwa " Kupiga Chabo"
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
akimtambulisha mwenyekiti wa muda wa kijiji cha Sayu,Paul Selena baada ya
aliyekuwepo kuondolewa kwenye nafasi kutokana na tabia yake ya kupiga
chabo-Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
*****
Mwenyekiti wa kijiji cha Sayu kata ya
Pandagichiza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini bwana Mataifa Balekele
(CCM) amesimamishwa kazi na wananchi wa kijiji hicho baada ya kudaiwa kuwa na
tabia ya kuwachungulia‘kupiga chabo’ wananchi wakiwa wamelala
majumbani mwao nyakati za usiku.
Uamuzi wa kumuondoa katika nafasi hiyo
umefikiwa na wanakijiji hao leo Novemba 3,2017 baada ya mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Josephine Matiro kufika katika kijiji wakati wa ziara yake kuzungumza
na wananchi kuhusu kilimo cha pamba.
Inaelezwa kuwa mwenyekiti huyo ambaye ana mke,watoto na
wajukuu amekuwa na tabia ya muda mrefu ya kuchungulia watu wakiwa wamelala
nyakati za usiku na pale wanaopigwa chabo wanapomkamata amekuwa akikiri kufanya
kosa na kuomba kuwalipa pesa ili kuwafidia.
Inadaiwa kuwa amewahi kupiga chabo katika miji zaidi ya mara
10 na anapokamatwa hudai kuwa kapitiwa tu na shetani na amekuwa akiwalipa fedha
kama fidia watu aliowachungulia.
Hoja kuhusu mwenyekiti huyo iliibuka ghafla baada ya mmoja wa
wakazi wa eneo hilo Daudi Kapela aliibua hoja ya mwenyekiti wa kijiji hicho
Mataifa Balekele kusimamishwa kazi na nafasi yake kukaimiwa na Paul Selena
aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Sayu katika kijiji hicho.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hatua ya kumvua uenyekiti,mbele ya
mkuu wa wilaya,Afisa Mtendaji wa kata ya Pangagichiza Denis Kimwaga alisema
uamuzi wa kumsimamisha kazi mwenyekiti huyo ulichukuliwa Oktoba 12,2017 baada
ya uongozi wa serikali ya kijiji kukaa na kujadili malalamiko kutoka kwa
wananchi wakimtuhumu mwenyekiti huyo kufika kwenye nyumba zao na kuanza
kuwachungulia.
“Kikao hicho kiliridhia mwenyekiti huyo asimamishwe kazi
kutokana na tabia yake hiyo huku yeye mwenyewe akikiri kufanya vitendo hivyo
akidai kuwa amepitiwa tu na shetani na kuomba kuwalipa pesa kama fidia watu
aliowachungulia”,alieleza Kimwaga.
Hata hivyo mbali na kuridhia maamuzi ya wananchi,Mkuu wa
wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro alimteua Paul Selena kukaimu nafasi ya
bwana Mataifa Balekele mpaka pale taratibu za uchaguzi mdogo zitakapofanyika.
“Huu ni muda wa kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo,hivi sasa
hatuwezi kufanya uchaguzi kuziba nafasi hii,namteua Paul Selena kukaimu nafasi
hii”,alisema Matiro.
Akizungumza kwa njia ya simu na Malunde1 blog kutokana na
kutohudhuria katika kikao hicho Mataifa Balekele alieleza kukubalina na uamuzi
uliofikiwa huku akikanusha kujihusisha na tabia ya kuchungulia watu ambapo
alidai hizo ni chuki binafsi tu za baadhi ya watu wasiopenda awe kiongozi wa
kijiji hicho.
"Viongozi wa kijiji na baadhi ya wale wa kata pamoja na baadhi ya watu hawapendi tu mimi niwe kiongozi,wananifuatilia sana,kama wanasema mimi huwa nachungulia watu,waulize walinikamata lini,mbona hawapigi mwano?,hata yule mwanamke aliyedai hivi karibuni kuwa nilimchungulia,nilikubali tu kumlipa ili kuepuka maneno",alisema Balekele.
"Viongozi wa kijiji na baadhi ya wale wa kata pamoja na baadhi ya watu hawapendi tu mimi niwe kiongozi,wananifuatilia sana,kama wanasema mimi huwa nachungulia watu,waulize walinikamata lini,mbona hawapigi mwano?,hata yule mwanamke aliyedai hivi karibuni kuwa nilimchungulia,nilikubali tu kumlipa ili kuepuka maneno",alisema Balekele.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisikiliza maelezo kutoka kwa Daudi Kapela
Wazee wa kijiji cha Sayu wakiwa katika kikao hicho
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimtambulisha mwenyekiti wa muda wa kijiji cha Sayu Paul Selena
Wanakijiji wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Wananchi wakiwa katika kikao hicho.
No comments