SAKATA LA WENYE VYETI FEKI…SASA SERIKALI KUWAFUNGULIA KANZI DATA WASIAJILIWE
SEKRETARIETI
ya Ajira katika Utumishi wa Umma imebainisha kuwa bado kuna baadhi ya waombaji
wa kazi za utumishi wa umma wanaoendelea kughushi sifa za kielimu, taaluma na
taarifa binafsi pamoja na hatua kali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali.
Kutokana
na taarifa hiyo, serikali imeagiza sekretarieti hiyo kufungua kanzi data ya
kutengeneza orodha ya watu wote wanaoomba ajira kupitia chombo hicho
watakaobainika kufanya udanganyifu kupitia vyeti vyao ili wawekewe zuio la
ajira za utumishi wa umma serikalini.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella
Kairuki aliagiza sekretarieti hiyo kuwachukulia hatua waombaji wote
watakaobainika kuwasilisha taarifa za taaluma zenye udanganyifu ikiwa ni pamoja
na kuanzisha kanzidata yenye orodha yao ili wawekewe zuio la ajira serikalini.
“Naomba
utaratibu uwekwe wa kuwasajili watu hawa wadanganyifu kupitia kanzidata na kuwa
‘black listed’ (kuwafungia), orodha hii ipelekwe kwenye ofisi zote na taasisi
zote za serikali ili wasipate ajira kwa njia yoyote, lakini pia washitakiwe kwa
kuthubutu kuja kwenye chombo kizito kama hiki na kudanganya,” alifafanua
Kairuki.
Aidha,
imebainika kuwa baada ya ajira kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18,
sekretarieti hiyo imepokea vibali vya ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya nafasi
2,611 na hadi kufikia Septemba mwaka huu, waombaji 185 wameshapangiwa vituo vya
kazi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa bodi mpya na Mkataba wa Huduma kwa Mteja ya Sekretarieti
hiyo ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Katibu wa Sekretarieti hiyo, Xavier
Daudi alisema kughushi vyeti bado ni changamoto wanayoendelea kukumbana nayo.
Daudi
alisema pamoja na chombo hicho kimeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na
kufuatilia vyeti hivyo vya kughushi vinapotolewa na kwamba imebaini taasisi
zinazotambulika zinazotoa vyeti hivyo.
“Hili
tumeliona hasa kwenye nafasi za udereva, kuna vyuo vya udereva vya mitaani tena
vilivyosajiliwa na Vyuo Ufundi vya Veta, tulipofuatilia na kuvihoji baadhi yake
kuhusu vyeti hivi vya kughushi vimekiri kuwa vyeti hivyo ni vyao.
Hili
ni tatizo kwa kweli,” alisema Daudi. Katibu huyo alisema baada ya ajira
kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18, sekretarieti hiyo imepokea vibali vya
ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya nafasi 2,611 na hadi kufikia Septemba mwaka
huu, waombaji 185 wameshapangiwa vituo vya kazi.
“Katika
juma lijalo tunatarajia kuwapangia vituo vya kazi zaidi ya wasailiwa 400 ambapo
pia tuna vibali vingi ambavyo vipo kwenye hatua mbalimbali,” alieleza. “Naomba
niweke wazi kuwa chombo hiki hakikuanzishwa kwa bahati mbaya, kilianzishwa kwa
ajili ya kutatua changamoto za ajira nchini kutokana na matatizo kadhaa
yaliyokuwepo huko nyuma kama vile kuajiri bila kuzingatia sifa, ukabila, udini,
undugu na urafiki, na gharama kubwa za matangazo ya ajira,” alieleza.
Pamoja
na hayo, waziri huyo aliagiza sekretarieti hiyo, kuhakikisha inafanya mchakato
wa ajira kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za ajira zilizopo na kupata
watumishi wa umma wenye sifa stahiki, hivyo kuisaidia Serikali kutekeleza
mipango yake ya kiuchumi na kimaendeleo.
“…Naomba
muendelee kuwa wabunifu na kutumia mbinu za kisasa katika kutekeleza majukumu
yenu ili rasilimali watu mnayoiandaa ikidhi matarajio ya wadau wenu pamoja na
taifa kwa jumla,” alisema Waziri Kairuki. Alisema chombo hicho kikitoa
wasailiwa bora wanaokidhi mahitaji ya waajiri, watasaidia taifa kufikia malengo
iliyojiwekea ikiwemo kuijenga Tanzania.
No comments