Breaking News

Watetezi haki za binadamu waitaka serikali kuzingatia misingi ya demokrasia, utawala wa sheria kutekeleza majukumu yake.

Image result for helen kijo bisimba
Mtandao wa mashirika ya Watetezi wa haki za binadamu nchini umeitaka serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala wa sheria ikiwemo uhuru wa vyama vya siasa.

Akisoma tamko la wadau hao katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Amani duniani ambayo udhimisha kila mwaka tarehe 21 septemba, Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu Dkt. Helen Kijo bisimba alisema amani ujengwa kwa kwa kufuata misingi ya tawala bora pamoja na kuzingatia misingi ya demokrasia.

Alisema misingi amani iliyopo nchini imechangia ustawa wa taifa kijamii, kisiasa na kiuchumi pamoja na kuwajengea watanzania utashi wa utu, mshikamano na uzalendo pamoja na kuwepo changamoto ambazo tunaendelea kuzikabili.

“Tunawapongeza watanzania kwa kuweza kudumisha amani yetu kwa miaka zaidi ya 50 tangu tulipopata uhuru 1961 na hata tulipongana na Zanzibar 1964 na hata mara baada ya kurejesha mfumo wa vyama vingi nchini” Alisema Dkt Bisimba.

Alisema pamoja na jitihada zote zinazochukuliwa za kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano uliopo nchini mashirika ya utetezi wa haki za binadamu wamebaini kuwepo na viashiria vinavyoweza kupelekea kutoweka kwa amani iliyopo nchini.

Amevitaja viashiria hivyo kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa utawala wa kisheria, kuongezeka kwa vitendo vinavyotia hofu kuhusu amani na ulinzi wa haki za binadamu, matukio ya ukamatwaji kihilela kwa wanasiasa na wafuasi hasa wa vyama vya upinzani pamoja na kuminya uhuru wa habari na uhuru wa maoni.

Alisema kufatia kubaini viashria hivyo mtandao wa mashirika ya watetezi wa haki za binadamu umeshauri vyombo vya usimamizi wa sheria kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wakati na weledi ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Aidha Dkt. BIsimba aliongeza kuwa serikali ichukue hatua za makusudi za kuhakikisha ustawi wa umoja wa kitaifa kwa kuyaunganisha makundi yote yanayosigana kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Maadhimisho ya siku ya Amani duniani ambayo uadhimishwa kila mwaka tarehe 21 septemba, mwaka huu 2017 yamebeba kauli mbiu ya “Pamoja Kwa Ajili Ya Amani: Nizamu, Usalama Na Heshima Kwa Wote”.

No comments