Meya Ya Jiji Mhe Mwita Aitumbua Kampuni Mwamkinga Auction Mart And Brokers
MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es
Salaam Isaya Mwita leo ametangaza kuvunja mkataba wake na kampuni ya Mwamkinga
Auction Mart and Brokers iliyokuwa ikifanya kazi ya kudhibiti uegeshaji wa
magari katika maeneo yasiyo rasmi katika Halmashauri ya Temeke na Kigamboni.
Meya Mwita amefikia uamuzi huo
kutokana na kampuni hiyo kufanya kazi zake kwa kutozingatia matakwa ya mkataba
na hivyo kusababisha kuanzisha migogoro isiyo ya lazima kati ya wananchi na
Halmashauri ya Jiji.
“Wakandarasi wetu lazima waheshimu hawa Watanzania
wanaotumia magari sio “ATM” nimesikia kelele nyingi sana kuhusu Mwamkinga jinsi
anavyokamata malori kule, kimsingi anawaotea na kuwapiga faini kubwa pengine
laki tatu hadi nne na watu wanakuwa wameegesha kwa dharura chini ya dakika 30
anawapiga faini”,
alisema Mwita.
Mstahiki Meya ameongeza kuwa
Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imeamua kusitisha mkataba huo kuanzia
Septemba 19 kwasababu ameshapewa onyo lakini hawajaonesha nia ya kubadilika.
Aidha Mwita amewataka
Wakandarasi wengine waendelee kufanya kazi kwa weledi vinginevyo atavunja
mikataba yao pia.
Amesema haiwezekani kwamba mtu
amesimama kwa dakika moja alafu gari lake linafungwa kwa mnyororo na
kumwandikia faini ya Sh 200,000 hadi Sh 300,000 ambayo haipelekwi
halmashauri.
“Hiyo kampuni ilikuwa inafanya kazi hadi saa tatu
usiku tofauti na makubaliano ya mkataba unavyosema mwisho saa 12 jioni.
Nitaendelea kufuatilia kwa wilaya za Kinondoni na
Ilala ambapo kama wataenda tofauti na mikataba inavyosema watasitishiwa
mikataba yao" ameongeza.
Mwita amesema lengo la
halmashauri siyo kumkandamiza mwananchi bali kusimamia sheria ili watu
wazifuate lakini imeonekana tofauti ambapo amekiri kusikia watu hao wanakusanya
hadi shilingi milioni nne kwa mwezi ambazo haziwasilishwi katika halmashauri ya
jiji.
No comments