TGNP Mtandao: Tanzania Kuna Mapungufu Makubwa Katika Utunzaji Wa Kumbukumbu Za Wanawake Waliochangia Maendeleo Ya Taifa
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule akizungumza
na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa TGNP Mtandao jijini Dar es salaam.
Dar es salaam:
Imebainika kuwa kuna mapungufu makubwa
nchini katika utunzaji wa kumbukumbu hasa za wanawake wanaochangia maendeleo ya
taifa licha ya kwamba wanawake wanachangia maendeleo bega kwa bega na
wanaume.
Akizungumza leo Septemba 8,2017 na
waandishi wa habari wakati wa kuhitimisha tamasha la 14 la Jinsia mwaka 2017
lililoanza Septemba 5,2017, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule
alisema kumbukumbu za wanawake waliochangia maendeleo ya taifa
hazijaandikwa.
Alisema katika tamasha hilo
lililokutanisha wadau zaidi ya 1500,wamekubaliana kuendelea kuimarisha mikakati
ya kuweka kumbukumbu za wanawake waliotoa michango katika maendeleo katika
nyanja mbalimbali.
Shule alieleza kuwa mbali na kutunza
taarifa hizo za kumbukumbu,pia watazisambaza kwa ajili ya watu kujifunza na
kuwaenzi wanawake hao pamoja na kutoa mafunzo ya kimwongozo katika kuchukua na
kuhifadhi kumbukumbu za wanawake kwa asasi za kiraia,vijana na wadau
wengine.
Hata hivyo alieleza kuwa kufuatia
utafiti mdogo uliofanywa na TGNP Mtandao,walibaini kuwepo kwa wanawake
waliochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa na kupitia tamasha hilo TGNP
iliwapatia wanawake hao tuzo ya kutambua michango yao.
Shule aliongeza kuwa tuzo hizo ni
sehemu ya mipango endelevu ya kurithisha ujuzi na maarifa kwa vizazi vipya
pamoja na kujifunza kwa wanawake na wanaume waliobobea katika Nyanja
maalum.
Wanawake hao walikabidhiwa tuzo hizo na
Makamu wa rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa tamasha la
Jinsia, Septemba 5,2017.
Aliwataja wanawake waliopewa tuzo kuwa
ni Mheshimwa Samia Suluhu,Getrude Mongella,Spika mstaafu wa bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,Anne Makinda,Profesa Daktari Esther Mwaikambo,Anna
Abdallah na Esther Bulaya.
Wengine ni wanachama wa TGNP Mtandao
waliotoa mchango mkubwa katika kujenga Tapo la Ukombozi wa wanawake kimapinduzi
akiwemo Profesa Marjorie Mbilinyi,Asseny Muro,Mary Rusimbi,Demere
Kitunga,Subira Kibiga,Aggripina Mosha na Zippora Shekilango.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP
Mtandao,Vicensia Shule
Washiriki wa tamasha la jinsia mwaka 2017 wakicheza leo
Septemba 8,2017 katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es salaam
No comments