Breaking News

Mbunge Wa CCM Asimulia A To Z CHADEMA Ilivyopata Ndege Ya Kumbeba Tundu Lissu Kumpeleka Kenya


Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky amefunguka na kusema CHADEMA ndiyo imelipa gharama za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Kenya na kusema yeye aliwadhamini wakati huo kwa kuwa hawakuwa na fedha taslimu za kulipa

Salim Hassan Turky ametoa ufafanuzi huo leo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Mbunge huyo ndiye aliyelipia gharama za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Kenya kwa matibabu, taarifa ambayo imetolewa na Spika wa Bunge jambo ambalo CHADEMA wamelipinga na kusema Spika anapotosha umma juu ya jambo hilo. 

“Tusifanye tukio la Tundu Lissu kuwa la siasa. Mimi binafsi tukio zima la mbunge mwenzangu limenisikitisha sana limenisononesha sana. Nikiwa kama kamishna wa Bunge lakini pia ni binadamu kuna kuzaliwa na kufa,”amesema.

“Kwa hiyo tukio hilo lilipotokea tuliitwa na makamishna wote na Spika wetu wakiwemo Mbowe (Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani) Msigwa na timu yake. Kwanza ndege ilikuwepo pale Airport ambayo ilikuwa imeshaagizwa na Bunge iko stand by kumpeleka moja kwa moja Muhimbili.”

Amesema walichoamua ni kuwa aende moja kwa moja Nairobi nchini Kenya lakini ndege hiyo haikuwa na kibali cha kwenda nchini humo na kwamba ili uweze kwenda nchini humo unalazimika kuwa na marubani wawili.

Hata hivyo, amesema Spika Ndugai alihangaika kupata kibali cha ndege iliyokuwepo uwanjani ili iweze kumpeleka mgonjwa Nairobi.

“Wakati mambo yote tayari rubani wa ndege akasema kuna kitu kinaitwa landing Instrument ambayo ile ndege haina kwa hiyo haitaweza kuruka,” amesema.

Amesema kutokana na majibu hayo waliingiwa na sitofahamu watafanya nini lakini yeye aliingia katika uzoefu wake aliopewa na Mungu kwa kutafuta ndege kwa ndugu zake ambao wanafanya nao biashara sana.

“Nikawaambia ndege ipo wakatoa nauli zao za ghali ghali kwa sababu tunajuana wakakubali kutusaidia kwa dola 9,200 pamoja na ambulance (gari la wagonjwa) mimi ndio niliyoita kwa kubaliana na Mbowe na Msigwa kwamba Turky haya mambo yasimamie baadaye…na ndicho kilichofanyika,” amesema.
Aidha Turky aliendelea kueleza kuwa walipofika nchini Kenya siku ya pili walipaswa kuwa ametoa fedha hizo lakini haikuwa hivyo mpaka leo Septemba 14, 2017 majira ya saa sita mchana alipowasiliana na wahusika aliambiwa kuwa CHADEMA walikuwa wameshalipa hizo fedha.

Mbali na hilo Turky amesema kuwa kauli ambayo Spika wa Bunge Job Ndugai ameisema leo bungeni haikuwa na tatizo kwani alikuwa amesema yeye ndiye amelipa hiyo fedha lakini CHADEMA wangekuja kuirudisha kwake, jambo ambalo anadai kama leo wasingeweza kulipa CHADEMA basi angelipa yeye fedha hizo kwa watu hao halafu yeye angekuja kumalizana na CHADEMA.

Pia katika kauli ambayo ametoa Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa amesema kuwa fedha hizo za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Nairobi nchini Kenya imelipwa na Watanzania ambao walikuwa wanachangia fedha za matibabu kwa Lissu pamoja na CHADEMA wenyewe na si mbunge wa CCM.


No comments