LHRC Kuwanoa Kisheria Wasichana Shinyanga Kupambana Na Maambukizi Ya VVU
Baadhi
ya wasichana na wanawake wadogo watakaofikiwa na mradi katika picha ya pamoja
wakati wa uzinduzi wilayani Kahama
******
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa
kushirikiana na Shirika la Kimataifa la IDLO kimezindua mradi wa Kuwajengea
Uwezo wa Kisheria Wasichana na Wanawake Wadogo mkoani Shinyanga ili Kuweza
Kuiwajibisha Jamii Kutoa Huduma Bora za Afya ya UKIMWI.
Katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika
Septemba 14 katika manispaa ya Shinyanga na Septemba 15 katika Halmashauri ya
Mji wa Kahama, makundi lengwa ya mradi huo ikiwemo wasichana na wanawake
wadogo, wazazi, viongozi wa serikali na Jamii kwa ujumla yameonyesha kuvutiwa
na malengo na matokeo tarajiwa ya mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga wakati wa kuzindua mradi huo Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga Bw.
Charles Maugila alisema ujio wa mradi huo katika Manispaa ya Shinyanga ni wa
kufurahiwa kwani mkoa wa Shinyanga kwa ujumla unakabiliwa na changamoto kubwa
ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI hususani kwa wasichana na wanawake wadogo.
“Kumekuwa na miradi mingi inayolenga
kukabiliana na ukatili wa kijinsia na UKIMWI lakini mradi huu ni wa kipekee kwa
vile unalenga kuwajengea uwezo wa kisheria wasichana na wanawake wadogo ambao
ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI waweze kuwajibisha jamii kwa kudai huduma bora za afya ya
UKIMWI” Alisema Maugila.
Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga Bw. Charles Maugila akikata
utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Dreams Innovation Challenge wilayani humo.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Katibu
Tawala wa wilaya hiyo, Bw. Anthony Ndanya ameitaka Jamii ya Kahama kushiriki
kikamilifu na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo ili kuweza
kufikia malengo ya mradi huo na kupata matoke tarajiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Bw. Ezekiel
Massanja alisema “kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2016,
ukatili wa kijinsia ukijumuisha ukatili wa majumbani, ukatili wa kingono, mimba
za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na vitendo vingine vya kikatili kwa watoto
na wanawake vimezidi kuongezeka maradufu mbali na kuwepo kwa sheria zinazolinda
kundi hilo.
Moja ya matokeo ya changamoto za ukatili kwa wanawake ni
kuambukizwa virusi vya UKIMWI”.
“Sambamba na ongezeko la vitendo vya
kikatili, Jamii inakosa uwezo wa kuwawajibisha watekelezaji wa vitendo vya
kikatili na kushindwa kukabilianan na madhara ya ukatili wa kijinsia kutokana
na ukosefu wa elimu ya sheria na namna ya kudai upatikanaji wa huduma bora za
afya” – Aliongeza Massanja.
Mradi huu ni moja ya miradi mingi ya Dreams
Innovation Challenge inayotekelezwa nchini. Mradi umejikita
kuwajengea uwezo wasichana wa miaka 15 hadi 24 na jamii kwa ujumla juu ya
masula ya kisheria, afya na ukatili wa kijinsia. Mradi unalenga kuwapa uwezo
wasichana kuiwajibisha jamii pale haki zao za msingi zinapokosekana hasa kwenye
masuala ya afya ya UKIMWI.
Lengo kuu la mradi ni kuimarisha uwezo wa
jamii kuboresha huduma za afya ya UKIMWI kwa wasichana na wanawake wadogo
kupitia mbinu ya uwezeshaji kisheria na uwajibikaji kijamii.
Mradi unalenga kufikia jumla ya wasichana
1000 wenye umri kati ya miaka 15 – 24. Wasichana 500 Shinyanga na 500 wilayani
Kahama. Wanufaika wengine ni pamoja na wanaume ambao ni wapenzi wa wasichana
hao, wazazi, watoto, vyombo vya sheria, wahudumu afya pamoja na jamii yote kwa
ujumla.
No comments