Mhe Lissu : Kama Wakenya Mngemchagua Odinga Mngekoma
Rais wa TLS na
Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu amefunguka na kusema wao kama CHADEMA
waliwaambia watu wa Kenya kuwa kama watarogwa na kumchagua Raila Odinga kuwa
Rais wa nchi hiyo wangekoma kwani aliweka wazi ataongoza kama Rais wa Tanzania.
Tundu Lissu anasema
kuwa katika uchaguzi uliofanyika nchini Kenya tarehe 8 Agosti 2017 unatoa
mafunzo mengi kwa Tanzania kwani Kenya wameweza kupiga hatua kubwa na kutoa
haki ya msingi ya kupiga kura kwa wafungwa na Raia wake waliopo nje ya Kenya
jambo ambalo Tanzania ni kitu kisichowezekana.
"Kenya
inatufundisha umuhimu wa kuwa na Katiba mpya, Katiba ya Kidemokrasia, Katiba
inayoweka uhuru kwa wale wanaoshiriki uchaguzi kwa kuweka utaratibu wa kuhakiki
taratibu za uchaguzi katika kila hatua na hilo ni jambo muhimu sana, lakini
Kenya inatufundisha umuhimu wa kuwa na Demokrasia tumeona wafungwa wakipiga
kura, tumeona waandishi wa habari wakiruhusiwa kuiingia gerezani kueleza umma
jinsi zoezi la upigaji kura linavyoendelea hata kwa watu ambao wamepata adhabu
kwa mujibu wa sheria za Kenya lakini kwetu sisi hicho kitu hakipo kabisa,
tumeona raia wanaokaa nje ya Kenya wameshiriki uchaguzi sisi hilo
haliwezekani" alisema Tundu Lissu
Aidha Tundu Lissu
amesema kwa mambo yote ambayo yameendelea Kenya katika uchaguzi yanatoa funzo
kuwa na mfumo wa Demokrasia lakini pia amegusia chama cha CHADEMA kuwa rafiki
na Chama Cha Jubilee na kusema siyo dhambi.
"Sisi kuwa na
chama rafiki Kenya wala siyo kitu cha ajabu sana, tuna chama rafiki Ghana
tunavyama rafiki kila mahali na wakati wa uchaguzi marafiki wanaungana mkono,
wakati wa uchaguzi ANC wanaunga mkono CCM, Museven na NRM yake wanaunga mkono
CCM na sisi kwenye uchaguzi huo wa Kenya tumeunga mkono Jubilee, na kwenye
uchaguzi huu wa juzi Raila Odinga aliwaambia waKenya kuwa wakimchagua ataongoza
nchi kama Rais wa Tanzania ilibidi tuwaambie Wakenya kuwa mtakoma"
alisisitiza Tundu Lissu
Katika Uchaguzi
uliofanyika tarehe 8 Agosti 2017 nchini Kenya tume ya uchaguzi nchini humo
ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa nafasi ya Urais kwa kupata kura
zaidi ya milioni nane huku mpinzani wake Raila Odinga na Muungano wa NASA
wakishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni sita.
No comments