MHE NCHEMBA: CHENGE, WEREMA ELEZENI MASLAHI YENU KATIKA MCHANGA WA MADINI
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ametaka wanasheria
wakuu wa Serikali wastaafu waeleze hadharani maslahi waliyonayo kwenye kampuni
za madini zinazosafirisha mchanga nje ya nchi.
Hatua
hiyo ya waziri imekuja siku chache baada ya wanasheria wakuu wastaafu
waliofanya kazi kwa nyakati tofauti wakati nchi ikiingia kwenye mikataba ya
madini ‘kujivua lawama’ kuhusu udanganyifu uliogunduliwa kuhusa sakata la
usafirishaji wa mchanga.
Wanasheria
hao wakuu wa Serikali wastaafu ni Andrew Chenge na Jaji Frederick Werema na amewataka wamwache Rais Dk.
Magufuli aendelee kulinda rasilimali za umma zisiliwe na watu wachache.
Mwigulu
amesema hayo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa
na mamia ya wananchi wa Tarafa ya Ndago, Jimbo la Iramba.
Alisema
Chenge na Werema kwa nyakati tofauti wakiwa wanasheria wakuu wa serikali,
pamoja na majukumu yao mengine, wameshiriki kusaini mikataba mikubwa mikubwa, ikiwamo ya
makampuni ya kuchimba madini.
“Kwa
akili ya kawaida tu, baadhi ya mikataba mikubwa, ikiwamo ya makampuni ya
madini, haikuwa sawa… ndiyo maana imelalamikiwa kwa muda mrefu.” alifafanua
Mwigulu, Mbunge wa Jimbo la Iramba.
Alisema
juzi juzi magazeti yameeleza kuwa akina Chenge na Werema wamedai kuwa Rais wetu
Magufuli amedanganywa na tume maalumu ya Profesa Mruma.
“Wao ndio waliosaini mikataba ambayo
imechangia Taifa kupoteza mabilioni ya fedha kupitia usafirishaji wa michanga
nje ya nchi. Sasa wamegeuka na kuwa upande wa pili wa watu waliosaini pamoja
mikataba hiyo mibovu. Nawashauri watoke hadharani…. waeleze wana maslahi gani
na kampuni wanazozitetea,” alifafanua zaidi.
Aidha,
Mwigulu amesema Chenge na Werema wakishindwa kuweka wazi maslahi waliyonayo,
basi ni vema wakakaa kimya na kumwacha Rais wa vitendo aendelee kuinyoosha
nchi.
“Hivi
ukimpa mtu kazi ya kuuza duka, halafu kila siku awe anakuambia hajauza kitu na
huku akilalamika kuwa kila siku anapata hasara. Unamshauri aachane na biashara
inayompatia hasara, haachi…anaendelea kuwepo tu, utamwalewaje. Si atakuwa si
mkweli, mwongo ananufaika na hilo duka,” alisema.
Akiijengea
nguvu hoja yake, alisema Chenge na Werema wanaishi Masaki, jijini Dar es
Salaam, hawa hawawezi au watakuwa wamesahau maisha ya Watanzania wengi maskini
waliopo vijijini. Hivyo wamwache Rais Magufuli ambaye ameonyesha uzalendo wa
kweli, aendelee kulinda rasilimali za umma.
Alisema kwa wao wanaomfahamu Rais Magufuli,
kwa hili la kuchokonoa kwenye madini na kubaini upotevu mkubwa wa fedha za
umma, ni mwanzo tu, kazi bado ipo mbele ya kuchokonoa zaidi ubadhirifu na wizi
wa mali ya umma katika sehemu mbalimbali.
Mwigulu ametumia fursa hiyo kuwaomba
Watanzania wazalendo wa madhehebu ya dini mbalimbali waendelee kumwomba Mungu
ampe Rais Magufuli afya njema na ujasiri wa kuziba mwinya yote inayotia hasara
Taifa letu.
No comments