KAULI YA WAZIRI SIMBACHAWENE KWA WAKUU WA MIKOA, WILAYA WANAOWEKA WATU KIZUIZINI
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amewaonya wakuu wa mikoa na wilaya
kutotumia vibaya madaraka yao ya kukamata watu walio kwenye himaya zao.
Ametoa onyo hilo leo (Ijumaa)
alipojibu maswali ya wabunge waliotaka kufanyika marekebisho ya sheria
inayowapa mamlaka wakuu hao ya kuwakamata na kuwaweka ndani wananchi
wanaowatuhumu kwa lolote.
Licha ya kubainisha kwamba sheria
hiyo haina tatizo, waziri amesisitiza: "Ukamataji unatakiwa ufanywe kwa
mtu aliyetenda kosa la jinai au anayehatarisha usalama. Isiwe kwa show-off tu.
Na mhusika anatakiwa kufikishwa mahakamani mara moja, asishikiliwe tu."
Amesisitiza kwamba wakuu hao ni
wawakilishi wa Serikali kwenye maeneo yao, hivyo hawatakiwi kutumia vibaya
madaraka waliyokasimiwa.
Katika siku za karibuni wakuu wa
mikoa na wilaya wamekuwa wakilalamikiwa kuwaweka watu kizuizini pasipo kuwa na
sababu za msingi, miongoni mwao wakiwamo waandishi wa habari.
No comments