KAULI YA WAZIRI MKUU MSTAAFU WARIOBA: MSAIDIENI RAIS TUSHINDE VITA YA RASILIMALI ZA NCHI,SUALA LA MAKINIKIA SIO LA CHAMA,WALA SIASA NI LA WATANZANIA WOTE
Wananchi hawahitaji mgawanyiko wa uongozi na malumbano wanataka
maendeleo.Msaidieni Rais tushinde Vita ya Rasilimali za nchi.
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt
John Pombe Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya kwanza na ya pili ya uchunguzi
wa makontena 277 ya mchanga wa madini (makinikia) yaliyokuwa njiani
kusafirishwa nje ya nchi na uchunguzi ulifanyika na kulibaini ndani ya mchanga
huo kuna dhahabu na madini mengine kwa asilimia kubwa.
Aidha, Mhe Rais amechukua hatua mbalimbali kulingana na ushauri
wa kamati husika, pamoja na maamuzi yake kama Rais. Kutokana na sakata
hilo.
Idara ya Habari-MAELEZO imepata fursa ya kufanya mahojiano na
Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mstaafu Mheshimiwa, Jaji Joseph Sinde Warioba katika ofisi zake zilizopo Osterbay
Jijini Dar-es-salaam.
SWALI: Ninanukuu maneno ya Baba wa
Tafa, Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere kuhusu raslimali za nchi na hususan
madini alisema: “Madini yetu tuliyonayo ni vema kuyaacha mpaka Watanzania
watakapokuwa na ufahamu wa kutosha wataamua kuyachimba” mwisho wa kunukuu nini
maana yake?
JIBU: Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika
mwaka 1961 Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokea nchi kama Waziri
Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru akiwa hana wataalamu zaidi ya madaktari 2 na
yeye mwenyewe ambaye alikuwa msomi kutoka chuo Kikuu cha Edinburg Uingereza.
Kwa hali hiyo, Mwalimu alikuwa sahihi usingeweza kuruhusu rasilimali za nchi
mfano madini kuchimbwa na wageni kutoka nje maana yake Watanganyika wangekuwa
watazamaji tu bila kufaidika na lolote.
Mwalimu alihakikisha anawekeza katika elimu ambayo ilikuwa bure
kuanzia msingi hadi chuo kikuu. Na elimu ndio msingi wa kuondoa Ujinga,
Umasikini na Maradhi. Alitambua Watanganyika wakielimika na kupata utaalamu wa
madini ikiwa ni pamoja na uchimbaji watakuja kuyachimba na kufaidika.
SWALI:Tanzania ni kati ya nchi
zilizobarikiwa kuwa na raslimali nyingi za kila aina kuanzia madini, gesi,
wanyamapori na hifadhi, misitu, milima, maporomoko ya maji, mabonde maziwa
makubwa kwa madogo, bahari ya hindi na raslimali za mazao ya uvuvi, nchi yenye
ardhi ya kutosha watanzania wenye uwezo wa kufanyakazi kwa ufanisi. Unadhani
nini tatizo letu na nini cha kufanya?
JIBU: Sioni kama kuna tatizo la msingi,
lakini ni suala la uelewa mara nyingi kuna watu ambao huamini viongozi wao kwa
kila kitu wanachosema. Lazima wananchi wawe makini kwa sababu tatizo la
watanzania ni maendeleo kila mwananchi ana kiu ya kutaka tufikie mahala pazuri
kama Taifa na mimi nakubaliana nao kabisa.
Tuna rasilimali nyingi, ambazo kimsingi tukiweza kuzishughulikia
kwa makini kama lilivyoshughulikiwa suala la mchanga wa madini tutakuwa mbali
sana kiuchumi.
Mosi, tuangalie rasilimali ya madini kwa mapana yake na
kushughulikia wawekezaji wa ndani na wale wa nje, Barick na Acaccia ni sehemu
ndogo sana ya madini, tuangalie wachimbaji wa ndani mfano Tanzanite ni aibu
madini yanachimbwa Manyara biashara hii inatokaje Mererani na kufanyika Nairobi
na New Delhi tujiulize kwa nini sio Arusha na Dar-Es-Salam.
Pili, upande wa rasilimali za maziwa makubwa tuliyonayo
Victoria, Tanganyika na Nyasa, Bahari ya Hindi kuanzia Moa mpaka Tanga kwa
kiasi gani tumeweza kutumia rasilimali za bahari maharamia wanakuja na meli zao
wanavuna tu na kuwatajirisha watu wengine. Mfano ziwa Victoria linategemewa na
wananchi wengi na sasa samaki hamna wamekwisha kwa sababu hatusimamii
rasilimali zetu ipasavyo. Maana suala sio kuvuna tu tunalindaje hizi rasilimali
zetu ili ziwepo leo kesho na vizazi vijavyo.
Tatu, Maliasili zetu za wanayamapori, mbuga za wanyama, vitalu
vya utalii unampaje mfanyabiashara kibali cha kuwinda miaka 99 yaani atumie
yeye, wanawe na wajukuu zake, watanzania watatumia lini, haya ni masuala ya
msingi kabisa ya kuangalia upya.
Nne, Ardhi Mwalimu alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vine
Watu, Ardhi Siasa Safi na Uongozi Bora. Mwalimu Nyerere aliona ardhi ndio
kilakitu hivyo vyote tulivyovitaja vipo ardhini pamoja na sisi wanadamu
tunaitegemea kwa kila kitu. Maeneo mengi yaliyotumiwa na watu kwa shughuli za
ufugaji aidha , yana matumizi mengine kama nyumba, kilimo cha mashamba makubwa,
na idadi ya watu inaongezeka ardhi ni ileile hii imesababisha migogoro ya
watumiaji wa asili wa maeneo hayo na wenye matumizi mengine tunatatuaje
changamoto hii.
SWALI: Kwa kuwa umebobea katika
masuala ya mikataba na sheria, ushauri gani unautoa katika masuala yote ya
raslimali za Tanzania? Nani anatakiwa kusimamia raslimali hizi kwa ufanisi?
JIBU: Hii sio suala la mjua sheria au
asiyejua, Mwanasheria lazima anazijua sheria ndio maana amepewa dhamana.
Linalojitokeza ni ukosefu wa maadili ya uongozi, imani, utiii, uwazi na
kutopenda nchi yako na Watanzania ambao wamekupa dhamana ya kusimamia jambo.
Ndio maana Mwalimu Nyerere aliweka miiko ya uongozi, maadili ya
uongozi kwenye Azimio la Arusha. Kila mwananchi alikuwa anaweza kujua kiongozi
huyu muadilifu au sio muadilifu na anachukuliwa hatua kabla mambo
hayajaharibika.
Lakini sio vema kumhukumu mtu kwa jambo lolote lile, ni vema
busara itumike kujua kilichotokea mfano hili suala la mchanga wa madini ya
makinikia.
Jambo la msingi ni kutafuta suluhu itakayotupeleka mbele, tuone
sera zetu zikoje na zinatusaidiaje kulinda rasilimali za Taifa, tunarekebisha
vipi kuondoa tatizo, sheria na utendaji kwa ujumla. Naomba watanzania tutoe
maoni na mawazo yatakayoboresha sera, sheria na utendaji au usimamizi wa
rasilimali husika. Tunaweza kurudisha miiko na maadili ya uongozi katika
kusimamia rasilimali za nchi, kila Mtanzania ajue sio mali yake ni ya
Watanzania wote lazima aitunze vinginevyo atahukumiwa kwa hilo.
SWALI: Ni ukweli usiopingika kuwa
kosa limeshafanyika kwa hili tuliloliona la mchanga wenye madini ya dhahabu,
ambapo mhusika ambaye ni mmiliki wa Kampuni inayobeba mchanga huo tangu 1998
hadi 2017 amewasili nchini kuonana na viongozi wakuu wa serikali, nini maoni
yako kuhusu hili?
JIBU Sisi hatukushughulika na uchimbaji wa
madini, lakini utafiti tulifanya na kujua madini yapo na kuna maeneo mengi
ambayo tumeweza kufanya vizuri tunapata mapato, lakini hatukupata mapato yote.
Lakini hili la mchanga sitaki kulizungumzia sana nadhani watu
wanalichukulia kwa mihemko sioni faida kuzungumzia matukio badala ya kuona
tafsiri nzima nini cha kufanya.
Ninachokiona na cha muhimu sana, Watanzania wamepata faida kwa
mara ya kwanza tumeweza kujua mikataba ya madini ikipitiwa na Kamati zote mbili
zimetueleza maeneo yote ya mikataba waliyopitia na kuja na mapendekezo.
Tumetambua serikali ilikuwa na hisa au la mrahaba asilimia ngapi, kodi kiasi
gani, na mambo kama hayo.
Naomba jambo hili lisibague, tunasema hatupati mapato ya kutosha
ni lazima tujue kwa wachimbaji wa nje na wa ndani mfano nani anajua wachimbaji
wadogo wadogo wamechimba madini kiasi gani tangu 1998 hadi 2017 na kodi kiasi
gani imeimngia. Tumepata nafasi sasa ya kuangalia sera za kulinda rasilimali ya
madini na nyingine zote katika nchi, kama maliasili ya bahari tunaitumiaje,
gesi, makaa ya mawe, chuma, wanyama pori na mambo kama hayo.
Hii imetufungua macho sera ya aina gani sheria za aina gani,
jinsi gani ya kutunza na kutumia rasilimali hizi tulizopewa na mungu.
SWALI: Kwa kuwa wananchi tulio wengi
tunaenda kwa mihemko bila kupambanua hoja husika na kutoa mapendekezo au maoni
yatakayo isaidia serikali kuboresha sera sheria na utendaji wa rasilimali zetu
unadhani tatizo ni nini?
JIBU: Hatujaona uongozi wa Kitaifa katika
hili suala la mchanga wa makinikia ninachokiona mimi ni uongozi wa chama na
siasa nyingi, sio sahihi kabisa wanafanya makosa hili ni suala la rasilimali za
nchi ni la kila Mtanzania.
Viongozi hawawatendei haki wananchi wanaowakilisha, wanakuwa na
mihemko wanasema kamata, shitaki, wafunge. masuala ya kitaifa hayaendi hivyo
sisi sio Polisi wala Mahakama waachieni wenye kazi yao.
Uongozi wa kulalamika hautusaidii, wananchi wanataka kuona
rasilimali zetu zinanufaisha na kuboresha huduma za jamii ambazo wanalalamika
kila leo hakuna dawa, elimu isiyowajenga vijana na mambo kama hayo.
SWALI: Mhe. Kutokana na sakata la
mchanga wa dhahabu uliokuwa unasafirishwa nje ya nchi na matokeo yake
watanzania tunajifunza nini kwa maoni yako?
JIBU: Kabla ya tuona funzo tulilopata
nadhani ni vema nikazungumzia jambo hili, nimeona mjadala katika mitandao ya
kijamii ambayo inafanywa kwa mihemko. Ukiangalia vyombo vya habari au viongozi
tumejikita katika majina ya watu, nilikuwa nnaangalia Bunge wote wanakwenda kwa
wale waliotajwa unakuta kuna wanaochangia na wanaolaumu ama unsahangilia au
unalalamika kuhusu watu.
Kubwa ni utaratibu tulionao haitasaidia kulalamika juu ya watu
waliofanya kazi huko nyuma, tunaweza kuwauliza wahusika nini kilitokea mpaka
kufanya hivyo, lakini hilo sio kubwa, muhimu ni kutafuta ufumbuzi.
Mjadala huu umenikumbusha Awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere
viongozi wote na wananchi walikuwa wanalalamika kila kitu wanachokikosa ni kwa
sababu ya wakoloni. Mwalimu akasema namnukuu: “Ni kweli wakoloni wametuleta
matatizo mengi sana lakini haitoshi kulaumu wakoloni bila kuondoa mateso ya
wananchi”. Mwalimu akaja na Waraka ambao ulikuwa unaitwa “Act dont Argue”
nadhani bado upo.
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi nanukuu
amesema. “Napenda kupata maoni tufanye nini kuhusu suala hili la mchanga wa
dhahabu (makinikia).” Namuunga mkono, sasa tumepata nafasi ya kutoa maoni,
mawazo ambayo ni muhimu sana maoni ya wadau katika uundaji wa sera na sheria
Sasa hivi siamini kama hatuna utaalamu, nina hakika tunao wa
kutosha tatizo ni maadili na hilo lazima kutafuta ufumbuzi wake, pia tuunge
mkono serikali inachofanya kupambana na rushwa na ufisadi.
“Lakini tusijidanganye bishara ya madini, mafuta ina changamoto
kubwa sana duniani hususan Afrika, maana unapambana na watu wenye fedha
biashara hii popote utakapo kwenda, ambapo uchumi unategemea mafuta na madini
utaona jinsi wakubwa wanavyooneemeka na rasilimali hizo na kuwaaacha wananchi
wakiwa masikini mfano mzuri Nigeria”.
Pamoja na kuangalia maadili na nidhamu lazima kuwe na uwazi
katika mikataba ni muhimu sana.
SWALI: Una maoni na mapendekezo yako
kwa viongozi wote na Mhe Rais katika kumuunga mkono?
Kwanza naliona hili la malumbano yatatugawa, waache tofauti zao
hii lawama ya madini ingekuwa ni mwanzo kwa kuleta mawazo na maoni ya
kutengeneza nchi yetu katika kulinda na kuzitumia rasilimali zote kwa maendeleo
ya taifa letu.
Viongozi msaidieni Rais kulishughulikia kwa pamoja hili si jambo
la chama wala Taasisi. Hakuna haja ya kupeana lawama ukishasema tumekosea
unatakiwa ueleze tufanye nini, sio kusema serikali ichukue hatua kwani serikali
ni nani si mimi na wewe sasa kwa nini hutaki wewe kulitolea maoni?
Tujiamini nimeona katika malumbano hayo, wengine wanaonekana
kama hatujiami kama tukifanya hivi tunaweza kushitakiwa, mabadiliko yoyote yana
machungu yake. Tusije tukapoteza imani tuliyonayo maana tunaweza tukapoteza
mapato yetu lakini ni lazima tufanye kwa kujenga afya ya rasilimali zetu.
Rais amekutana na mmiliki wa Barick na kila upande una msimamo
wake, tuiachie serikali na nina imani kabisa serikali itafanikiwa.
Kinachonishangaza ni mazungumzo ya baadhi ya viongozi kuwa serikali ihakikishe
tunapata hizo fedha walizo taja kwenye taarifa.
Nadhani hii sio sahihi, tuna imani na Viongozi wet wakuu haswa
Rais, lolote litakaloafikiwa tulipokee na kulikubali tusije kuanza kulumbana
ripoti imesema trilioni 108 ziko wapi? Pia nilisemee hili la dalili za kupoteza
imani, eti tukifanya hivyo tutashitakiwa, sababu ya mikataba na wawekezaji
hawatakuja mimi naamini watakuja tu rasilimali zipo kwetu hawana jinsi.
SWALI: Msaada wako binafsi kwa Rais
au maoni yako kwa Rais
JIBU: Sisi tupo, Uongozi ni suala la kupeana vijiti mimi natoka
Mara nimepitia utamaduni wa kabila langu kwa utamaduni wetu unafika mahali
unangatuka watu wanadhani kungatuka ni kustaafu hapana sio sahihi. Ukitoka
jandoni mzee wako lazima angatuke maana umekuwa sehemu ya jeshi la kabila na
yeyote ambaye kijana wake yuko kwenye jeshi yeye anatoka.
Wazee hawaingii katika mambo ya vijana na sisi tupo lakini
hatutaki kuingilia utendaji wao kama sisi tulivyoachiwa kuendesha nchi, ila
Rais akituhitaji tupo tayari kwa ajili ya ushauri anaweza kuukubali au
kuukataa. Nataka nimhakikishie kwa hili tupo pamoja na tutatoa maoni ya
kurutubisha Sera, Sheria na Utendaji katika rasilimali za nchi hii.
Source Habari Maelezo
Dar
No comments