MAALIM SEIF ‘AMCHONGEA’ LIPUMBA KWA GWAJIMA
Katibu Mkuu wa Chama
cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameutua mgogoro wa chama chake kwa
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima huku kiongozi huyo
wa kidini akitangaza kuwa atamlipua Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba Jumapili
ijayo.
Akizungumza Dar es
Salaam jana wakati alipomtembelea Askofu Gwajima, Maalim Seif alibainisha
kwamba amemweleza kiongozi huyo mambo mbalimbali ikiwemo suala la mgogoro ndani
ya CUF, aliodai umesababishwa na Lipumba.
Alisema kuwa ameamua kwenda
kwa Askofu Gwajima kumweleza hayo kwa sababu ni rafiki yake na hawajaonana siku
nyingi lakini pia kiongozi huyo alikuwa haelewi mgogoro wa CUF umesababishwa na
nani.
"Nimemweleza
Askofu Gwajima mambo mengi hususani mgogoro wa CUF hivyo ataamua mwenyewe nini
afanye kutokana na niliyomweleza,"alisema.
Aliongeza kuwa mbali na
kwenda kwa Gwajima pia ameshazungumza na
viongozi wengine wa dini husuani ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Askofu
Gwajima alisema kuwa ameshafahamu chanzo cha mgogoro huo kwa kuwa Maalim ni
rafiki yake wa siku nyingi lakini Lipumba hana urafiki naye.
"Mimi huyu ni
rafiki yangu kwa hiyo nilitaka kujua Professa Lipumba anafanya nini kuvuruga
CUF, hivyo nilitaka kujua Lipumba amepatwa na nini mpaka amevuruga chama chako
na kiukweli mimi nilikuwa siufahamu vizuri huu mgogoro ila saizi Seif
ameniambia kwa hiyo na mimi nataka nitafakari alichoniambia rafiki yangu ni
‘digest’ baada ya hapo nitajua nafanya nini” alisema Gwajima
Alipoulizwa kama watu
watarajie chochote kutokea kuhusu CUF, Maalim Seif na Lipumba kwenye ibada
Jumapili ijayo, Gwajima alijibu: “Kumbe mnajua, subirini Jumapili ifike
nitamlipua na tutajua amekula maharage ya wapi.”
No comments