SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI ATOA NAFASI YA MWISHO CHADEMA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa nafasi ya pili
na ya mwisho kwa ajili ya mchakato wa kuwapata wawakilishi wawili wa Tanzania
katika Bunge la Afrika Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Akitoa taarifa yake bungeni leo , Spika wa Bunge hilo Job Ndugai
amesema hadi sasa nafasi hizo bado ni za CHADEMA na atahakikisha haki hiyo
wanaipata na kwamba Katibu wa Bunge atatoa taarifa ni lini mchakato huo
utafanyika.
Katika hatua nyingine, Ndugai ametoa tahadhari kwa chama hicho
kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa utaratibu wa kupatikana kwa wawakilishi
wa Tanzania kupitia vyama vya upinzani, hivyo endapo wasipotumia nafasi hiyo,
atatumia mamlaka aliyonayo kutangaza utaratibu mwingine ili Tanzania isikose
wawakilishi katika nafasi hizo.
“Ikumbukwe kuwa maamuzi haya ya
kuwatenganisha wabunge wa upinzani kwa kuangalia vyama vyao ni maamuzi ya
Spika, tukumbuke mabunge yaliyopita maspika wenzangu hawakufanya hivyo,
waliwaweka wabunge wote wa upinzani kwenye kundi moja, mimi nikasema twende na
demokrasia hii ya wawili, ambayo katika kufanya hivyo, mimi
yuleyule,....tuendelee....... Hatuwezi kukubali nchi yetu ikose uwakilishi nchi
yetu ikatekwa nyara kwa sababu fulani fulani". Amesema Ndugai
Pia Ndugai amewatoa hofu watanzania kuwa hawatakosa uwakilishi
kwa kuwa anajua cha kufanya. "Tutatoa
nafasi ya pili, lakini baada ya nafasi ya pili, tunajua hatua itakayofuata,
nawahakikishia watanzania kwamba hawatakosa nafasi katika bunge hilo”
Katika uchaguzi uliofanyika juzi, Bunge hilo liliwachagua
wajumbe 7 kati ya 9 waliohitajika, huku wagombea wawili wa CHADEMA
Ezekiah Wenje na Lawrence Masha wakikataliwa kwa kupigiwa kura za hapana.
No comments